VIDEO: Kikosi cha kwanza cha Yanga chaingia na Coaster Taifa

Muktasari:

  • Mabaunsa wa Yanga walionekana kuwa imara kulinda eneo lao ili mashabiki wa Simba wasisogee eneo hilo.

Si unajua kuwa leo kuanzia saa 10 jioni mechi kati ya Simba na Yanga inachezwa pale Uwanja wa Taifa.

Basi kama ulikuwa hujui, kikosi cha kwanza cha Yanga kimeingia uwanjani hapo na basi aina ya Coaster, tofauti na ilivyozoeleka kwa wachezaji wote wa timu hiyo kuingia na basi kubwa.

Yanga ndio wamekuwa wa kwanza kufika uwanjani hapo, huku gari kubwa lililokuwa limebeba baadhi ya wachezaji wake likipitiliza sehemu lililopozoeleka kupaki na kwenda kusimama karibu na mlango wa kuingilia mashabiki wa Simba.

Saa 7:53 mchana gari aina ya Toyota Coaster liliingia uwanjani huku likiwa limebeba wachezaji ambao wataanza kwenye mechi ya leo.

Wachezaji wa Yanga waliingilia mlango usio rasmi jambo lilozua kelele kwa mashabiki wa Simba.

Basi lao kubwa liliwabeba kocha wa makipa Juma Pondamali, meneja wa timu Nadir Haroub 'Cannavaro' baadhi ya wale ambao wanabeba vifaa vya wachezaji.

Baada ya wachezaji wao kushuka na kuingia vyumbani kwenye mlango usio rasmi Cannaro na Pondamali waliwafuata na kuingilia mlango huo.

Mabaunsa wa Yanga walionekana kuwa imara kulinda eneo lao ili mashabiki wa Simba wasisogee eneo hilo.