Kilimanjaro Queens yafuzu kibabe nusu fainali Chalenji

Muktasari:

Kili Queens kuongoza Kundi A, ikiwa na pointi sita na mabao 13, wakifuatiwa na Burundi yenye pointi tatu na mabao matano sawa Sudan Kusini iliyo ya tatu na Zanzibar inashika mkia

Dar es Salaam.Timu soka ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Queens' imefuzu kibabe kucheza hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Chalenji baada ya kuichapa Burundi kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kilimanjaro Queens ikicheza mbele ya maelfu ya mashabiki wake ilitawala mchezo huo tangu mwanzo na kufanikiwa kupata ushindi huo wa kishindo.

Kilimanjaro ilipata mabao yake kupitia kwa Donisia Minja alifunga mabao mawili katika dakika ya 36, 65, huku Asha Rashid 'Mwalala' alipachika la tatu dakika ya 72 na Mwanahamisi Omary 'Gaucho' akamaliza dakika ya 86.

Ushindi huo unaifanya Kili Queens kuongoza Kundi A, ikiwa na pointi sita na mabao 13, wakifuatiwa na Burundi yenye pointi tatu na mabao matano sawa Sudan Kusini iliyo ya tatu na Zanzibar inashika mkia haina pointi wala bao.

Tanzania Bara itasubiri mshindi kati ya Sudan Kusini na Burundi ili kupata timu ya pili watakayoungana nayo katika nusu fainali.