Kipa Mbao asimulia bao la Ajibu

Mchezaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu, akifunga bao kwa mpira wa ‘tik tak’ katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Timu ya Yanga imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuilaza Mbao FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Tukio lililobeba sura ya mchezo huo ni bao la pili lililofungwa dakika ya 90 na kiungo Ibrahim Ajibu kwa mpira wa ‘tik tak’ uliomshangaza kipa wa Mbao Hashimu Mussa.

Dar es Salaam. Kipa wa Mbao, Hashimu Mussa amesimulia mpira wa bao la ‘tik tak’ la mchezaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu ulivyotinga wavuni.

Mbao ilikwaa kisiki katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuchapwa mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Mussa alisema hakuwahi kufungwa bao la aina hiyo katika historia yake ya soka na ameshangazwa na kipaji cha Ajibu.

Mussa alisema hakumbuki mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, alifunga kwa namna gani bao hilo la pili akitanguliwa Raphael Daud.

Ajibu alifunga bao maridadi kwa mpira wa ‘tik tak’ dakika ya 90, baada beki Amos Charles kushindwa kumdhibiti katika eneo la hatari.

“Sikutarajia kufungwa lile goli, lilikuwa tukio la haraka, binafsi nilishtuka kuangalia mpira uko wavuni hata jinsi ya kucheza ilikuwa vigumu kwa namna mpira ulivyopigwa,” alisema Mussa.

Kocha wa Mbao, Amri Said alisema kwa namna mpira wa Ajibu ulivyopigwa, ilikuwa kazi ngumu kipa huyo kuokoa shuti hilo la kushitukiza.

Ajibu alidokeza siyo mara ya kwanza kufunga kwa ‘tik tak’ kwa kuwa amekuwa akifunga mara kwa mara katika mazoezi ya kikosi hicho.

“Hakuna kocha anayekufundisha namna ya kufunga, mchezaji mwenyewe unajiongeza, yeye anakupa mbinu za kupata nafasi ya kufunga hata mimi jana (juzi) nilijiongeza,” alisema Ajibu.

Mabao mengine makali yaliyofungwa wikiendi iliyopita ni lile la Awadh Juma aliyeifungia African Lyon kwa shuti kali la mbali nje ya 18, Simba iliposhinda mabao 2-1 Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia kiungo nyota wa Arsenal, Aaron Ramsey alifunga bao maridadi kwa kisigino katika mchezo wa Ligi Kuu England ambao timu hiyo ilishinda mabao 5-1 dhidi ya Fulham.