Kipigo Man United chamliza Solskjaer

Muktasari:

  • Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, amedai matokeo mabaya iliyopata timu yake dhidi ya West Ham United yamemuumiza.

London, England. Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, amesema ameumizwa na matokeo ya jana kwa kuwa hakutegemea.

Man United iliduwazwa na West Ham United, baada ya kulala mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Matokeo hayo yamewaibua wachambuzi na nyota wa zamani wa Man United ambao wamesema timu hiyo inatakiwa kufanyiwa maboresho katika usajili wa dirisha dogo.

Solskjaer alisema matokeo hayo ni mabaya na hayakubadiliki kwa ustawi wa klabu hiyo ya Old Trafford.

“Nimesikitishwa na matokeo haya. Siku zote mtu anaumizwa  anapofungwa. Huu ulikuwa mchezo ambao tulipaswa kushinda lakini matokeo yamekuwa tofauti,”alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa timu hiyo.

Kocha huyo alisema Man United ina tatizo katika umaliziaji kwa kuwa imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini washambuliaji wanakosa umakini.

Kuumia kwa mshambuliaji wake tegemeo Marcus Rashford katika mchezo wa jana, kulionekana kuigharimu timu hiyo kwani ilishindwa kufunga licha ya kupata nafasi.

Solskjaer alisema anakubaliana na matokeo na anakwenda kujipanga kwa mechi zinazofuata.

Hata hivyo, alisema amepokea matokeo hayo kwa mtazamo chanya na anajipanga kukabiliana na changamo zinazoikabili Man United.

Man Utd itakuwa Old Trafford kuikabili Arsenal Jumatatu Septemba 30 katika mchezo wa Ligi Kuu England.