Kipigo cha TP Mazembe kwa Simba chadaiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi

Muktasari:

  • Mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Geitasamo amekufa akidaiwa kujinyonga chanzo kikitajwa kuwa ni Simba kufungwa na TP Mazembe.

Serengeti. Mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Geitasamo wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Emmanuel Ikwabe (13) amekufa kwa kujinyonga chanzo kikidaiwa ni timu ya Simba kufungwa na TP Mazembe.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Jumamosi iliyopita ya Aprili 13, 2019 majira ya saa 2:00 usiku nyumbani kwa Fanuel Mnanka ambaye ni baba yake.

Katika mchezo wa Klabu Bingwa Barani Afrika hatua ya robo fainali uliochezwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya DRC Congo Aprili 13, 2019 Simba ilitolewa na TP Mazembe baada ya kubugizwa mabao 4-1.

Mkuu wa polisi wilaya ya Serengeti, Methew Mgema akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili 16, 2019 amesema taarifa za awali waliambiwa kuwa baada ya Simba kufungwa mtoto huyo aliamua kujinyonga.

Amesema baada ya askari kufuatilia hakuna aliyejitokeza kutoa taarifa kuhusu chanzo cha kifo hicho na kuruhusu mwili kuzikwa jana Jumatatu Aprili 15, 2019.

Amesema wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Naye mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu amekiri kupata taarifa na kwamba uchunguzi zaidi unafanywa kubaini chanzo cha kifo hicho.

Mganga wa zahanati ya  Rung’abure, Samson Chacha amesema katika uchunguzi kwa kushirikiana na polisi walibaini kuwa alijinyonga.

Hata hivyo, Chacha hakutaka kueleza kwa undani kuhusiana na walichobaini kwa madai kuwa taarifa aliikabidhi polisi.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Geitasamo, Prospa Kirigini, amekiri aliyekufa ni mwanafunzi wake wa darasa la tano.

Hata hivyo, Kirigini amesema eneo waliloonyesha kuwa alilitumia kujinyonga linazua maswali kwa kuwa ni karibu sana kiasi kwamba angekuwa amegusa chini.

Mmoja wa majirani jina limehifadhiwa amesema shingoni hapakuwa na dalili za kujinyonga na kuwa uchunguzi wa mwili wote ulitakiwa kufanyika kabla ya mazishi ukweli ungejulikana.