Kisa kipigo Arsenal yamtwisha zigo Pepe

Tuesday October 22 2019

 

London, England. Winga wa Ivory Coast Pepe anapitia kipindi kigumu baada ya juzi usiku kushindwa kuinusuru Arsenal na kipigo dhidi ya Sheffield.
Arsenal ikiwa ugenini ilichapwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England, matokeo ambayo yamemuweka kikaangoni Pepe.
Licha ya kununuliwa kwa bei mbaya Pauni 72 milioni, Pepe ameshindwa kutamba Arsenal tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Lille ya Ufaransa.
Pepe aling’ara katika Ligi Kuu Ufaransa alipofunga mabao 35 katika mechi 74 alizocheza Lille kabla ya kujiunga na Arsenal katika usajili wa majira ya kiangazi msimu uliopita.
Winga huyo mwenye miaka 23, amefunga bao moja kwa penalti katika mechi tisa alizocheza Arsenal.
Juzi alikosa nafasi za kufunga licha ya mara kwa mara kuingia ndani ya eneo la wapinzanin wao.
Wakati Pepe akishindwa kutamba, kocha wa Arsenal Unai Emery alidai timu yake ilistahili kupata matokeo mazuri kwa kuwa ilicheza kwa kiwango bora.
“Tulistahili kupata matokeo mazuri. Nadhani kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini hatukuzitumia. Tulipata kona za kutosha pia hatukuzitumia,”alisema Emery.
Kocha huyo wa zamani wa Valencia na Paris Saint Germain (PSG) yuko kikaangoni baada ya mashabiki kuanza kumuandama kwa maneno makali wakimtaka ajiuzulu kutokana na mwenendo mbaya wa Arsenal msimu huu.

Advertisement