Kocha Arsenal aivulia kofia Watford

Monday September 16 2019

 

London, England. Kocha wa Arsenal Unai Emery amedai Watford ilikuwa bora zaidi yao katika mchezo walitoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Arsenal jana iliduwazwa baada ya Watford kupata penalti dakika ya 81 iliyofungwa na Roberto Pereyra. Bao jingine lilifungwa na Tom Cleverley.

Nahodha wa Gabon, Pierre Emerick-Aubameyang, aliyekuwa  nyota wa mchezo, alifunga mabao mawili ya Arsenal.

“Kwa utimamu wa mwili walikuwa bora zaidi yetu. Tuna vijana wadogo wanaendelea kujifunza na wanapata uzoefu kama huu wa leo (jana),” alisemas Emery.

Kocha huyo wa zamani wa Paris Saint Germain (PSG), alisema  wamefanya makosa na wanatafuta namna ya kurekebisha.

Kocha wa Watford, Sanchez Flores alidai amevutiwa na kiwango bora cha wachezaji wake waliocheza kwa kujiamini.

Advertisement

“Nimefurahishwa na matokeo haya, kupata pointi moja mbele ya timu ngumu kama hii si jambo rahisi. Matokeo yanatupa hali ya kujiamini,” alisema Flores.

Hii ni mara ya kwanza baada ya kupita miaka 22 kwa timu hizo kutoka sare katika mechi za mashindano yote ambapo mara ya mwisho zilitoka 1-1 Desemba, 1984.

Arsenal imeshindwa kupata ushindi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016 ikiwa mbele kwa mabao mawili, mara ya mwisho ilitoka sare 3-3 dhidi ya West Ham United.

Watford itakwenda Etihad kuikabili Manchester City Jumamosi wiki hii, wakati Arsenal itavaana na Eintracht Frankfurt ugenini katika mechi ya Ligi ya Europa, Alhamisi kabla ya kuivaa Aston Villa, Jumapili.

Advertisement