#WC2018: Kocha Croatia amshika uchawi mwamuzi Muargentina

Tuesday July 17 2018

 

Moscow, Russia. Kocha Zlatko Dalic amesema Croatia imecheza kwa kiwango bora licha ya kufungwa mabao 4-2 na Ufaransa katika mchezo wa fainali.

Dalic alidai bao la pili lililofungwa kwa penalti iliyotolewa na mwamuzi Nestor Pitana raia wa Argentina alidai ilikuwa ya kutatanisha liliwaondoa katika mchezo.

“Naipongeza Ufaransa kwa namna fulani, tulicheza vyema kwa dakika 20 za mwanzo na tulimiliki mpira, lakini bao la kujifunga na mkwaju wa penalti ulituvuruga

“Tafadhali usichukue kauli yangu kama sehemu ya kumlaumu mwamuzi, najaribu kutoa mawazo yangu, hakuna jambo lolote baya nyuma,” alisema Dalic.

Ivan Perisic alishika mpira ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Nestor Pitana aliamuru penalti baada ya kujiridhisha katika marudio ya teknolojia ya video ‘VAR’.

Mshambuliaji nguli Mario Mandzukic alijifunga bao la kwanza dakika ya 18 alipojaribu kupiga mpira kichwa uliotokana na adhabu iliyopigwa na Antoine Griezmann.

Dalic alisisitiza wachezaji wake walipambana na wanastahili pongezi kwa mchezo mzuri uliowafurahisha mashabiki wa soka mjini Moscow.

Pia kocha huyo aliipongeza Ufaransa kutwaa ubingwa, lakini hawakufua dau mbele ya vijana wake aliodai walicheza kufa au kupona kuipigania Croatia.

Kocha huyo alisema Croatia ilicheza vyema mechi ya fainali kuliko mchezo wowote nchini Russia.

Advertisement