Kocha Liverpool, Klopp awatisha Atletico Madrid wajiandae kwa mapokezi ya Anfield

Muktasari:

  • Liverpool ilishindwa kupiga hata shuti moja lililolenga goli dhidi ya ukuta bora wa Atletico. Hii ni mara ya pili kwa Liverpool kushindwa kumjaribu kipa wa timu pinzani tangu Klopp alipoichukua timu hiyo 2015.

Madrid, Hispania. Kocha Jurgen Klopp ameihadhalisha Atletico Madrid wajiandae na mapokezi magumu Anfield kulipa kilichofanywa Wanda Metropolitano wakati Liverpool ikipokea kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa.

Bao la dakika ya nne la Saul Niguez lilitosha kuipa Atletico ushindi muhimu nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool.

Uwanja wa Wanda Madrid ulikuwa umelipuka kwa shangwe za mashabiki jambo lililowapa nguvu vijana wa Diego Simeone.

"Mashabiki wa Atletico watakaopata tiketi... 'karibuni Anfield'," alisema Klopp.

"Mazingira ni jambo muhimu. Usiku huu walitimiza wajibu wao kwa upande wa Atletico, lakini sasa nataka kuweka malengo katika mchezo wa marudiano.

"Tumekuwa tukisema kila wakati kuhusu nguvu ya Anfield na uwezo wa uwanja wa nyumbani tumeona usiku huu.

"Tunakwenda mapumziko tulikuwa nyuma kwa bao 1-0. Kipindi cha pili tutacheza kwenye uwanja wetu na wao wataona kitakachotokea."

Liverpool ilishindwa kupiga hata shuti moja lililolenga goli dhidi ya ukuta bora wa Atletico. Hii ni mara ya pili kwa Liverpool kushindwa kumjaribu kipa wa timu pinzani tangu Klopp alipoichukua timu hiyo 2015.

"Sina tatizo na matokeo haya," aliongeza Mjerumani huyo, ambaye hajawahi kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ulaya akiwa na Liverpool. "Nimeona sura nyingi zenye furaha hapa Atletico, lakini mechi bado haijaisha.

"Sijui nini kitakachotokea katika mchezo wa marudiano. Watakuwa wamekwenda kuongeza petrol na sisi tutaendelea na safari tukiwa na tanki moja la mafuta.