Kocha Liverpool aitega Bayern Munich

Muktasari:

  • Kocha wa Liverpool, Jurgen  Klopp amesema mchezo wa leo dhidi ya Bayern Munich utakuwa wa aina yake kwa kuwa anakutana na timu bora Ujerumani.

London, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema ana furaha kuwa sehemu ya mechi kali ya leo usiku ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani.

Liverpool itakuwa mwenyeji wa Bayern Munich katika mchezo huo unaokutanisha wachezaji wenye viwango bora.

“Nina furaha kuwa sehemu ya mechi inayokutanisha timu mbili bora duniani,” alisema Klopp.

Kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alisema mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa unakutanisha timu bora na siku zote anaitazama Bayern Munich kwa jicho la tahadhari.

Klopp alisema amekuwa akichukua tahadhari kubwa katika mchezo dhidi ya Bayern Munich tangu akiwa Ujerumani.

Katika mchezo huo, Klopp atamkosa Roberto Firmino ambaye ni majeruhi lakini anatarajia kumtumia Daniel Sturridge katika safu ya ushambuliaji.

“Kuifunga Bayern Munich ni changamoto kubwa,” alisema Klopp ambaye mwaka 2008 aliwahi kutakiwa na klabu hiyo alipokuwa kocha wa Mainz.

Mchezo mwingine wa leo usiku, Barcelona itakuwa ugenini Ufaransa itakapovaana na Lyon.