Kocha Serengeti Boys awatoa hofu Watanzania

Monday April 15 2019

 

By Thobias Sebastian, Mwanachi

Dar es Salaam. Licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, Kocha wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, Oscar Mirambo amesema Tanzania ina nafasi ya kufanya vyema katika michuano hiyo.

Mirambo alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuanza vibaya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa kufungwa mabao 5-4 dhidi ya Nigeria.

Mchezo huo wa ufunguzi ulichezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi.

Mirambo alisema wachezaji walicheza vizuri ingawa kuna kasoro kwa baadhi ya maeneo hasa safu ya ulinzi na golini.

“Bado tuna nafasi kubwa ya kushinda mechi mbili zijazo, hiki ndio kitu kikubwa kwetu ambacho tunakifikiria kwa sasa. Jambo la msingi kwetu ni kuhakikisha watoto wanarejea kwa haraka katika hali zao,” alisema Mirambo.

Alisema benchi la ufundi litafanyia kazi kasoro zilizojitokeza hasa kwa upande wa kipa.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Vijana TFF, Lameck Nyambaya aliwataka wachezaji wa Serengeti Boys kusahau yaliyopita na kuangalia mchezo unaofuata kwa kuwa si wakati wa kujitafakari kupoteza mchezo huo.

Serengeti Boys itacheza na Angola keshokutwa Jumatano kabla ya kumaliza mechi yake dhidi ya Uganda Aprili 20.

Katika mchezo wa jana, safu ya ulinzi ya Serengeti Boys ilishindwa kuhimili kasi ya washambuliaji wa Nigeria.

Pia kipa Mwinyi Abdallah alionekana kushindwa kucheza kiki za mbali zilizopigwa na washambuliaji wa Nigeria.

Mchezo wenyewe

Dakika ya 20 Nigeria ilipata bao lililofungwa na Olatomi Olaniyan aliyekutana na mpira uliopigwa na kupanguliwa na kipa Mwinyi. Dakika moja baadaye Serengeti Boys ilisawazisha bao hilo kupitia kwa mchezaji Edmund John.

Nigeria ilipata bao la pili dakika ya 29 kupitia kwa Wisdom Ubani baada ya mabeki wa Serengeti Boys Mustapha Nankuku, Alphonce Msanga na Misungwi Chananja kukosa umakini katika kukaba. Nigeria ilipata bao la tatu dakika ya 36 lililofungwa na Akinkunmi Amoo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Serengeti Boys ilipata bao la pili dakika ya 51 lililofungwa na Kelvin John kwa kiki ya mbali.

Serengeti iliongeza kasi ya mashambulizi na beki wa Nigeria alifanya madhambi na mwamuzi aliamuru penalti iliyofungwa na Dominick William dakika ya 56.

Dakika ya 59 Serengeti Boys ilipata penalti baada ya beki wa Nigeria kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari na Edmund alifunga.

Hata hivyo dakika ya 78 Ibraheem Jabaar alipiga kiki kali ya mbali iliyomshinda kipa Mwinyi na mpira kujaa wavuni ulioipa Nigeria goli.

Serengeti Boys: Mwinyi Abdallah, Arafat Swakali, Mustapha Nankuku, Alphonce Msanga, Misungwi Chananja, Edmund John, Kelvin John, Pascal Msindo, Dominick William/Agiri Ngoda, Ally Rutibinga na Morice Abraham/Ladaki Chasambi.

Nigeria: Seleman Shaibu, Shedrack Tanko, Ogaga Oduku, Samson Tijani, Clement Ikenna, David Ishaya, Olankule Olusegun, Mayowa Abayomi, Wisdom Ubani, Akinkunmi Amoo na Olatomi Olaniyan.

Advertisement