Kocha Sven kukutana na mastaa Simba SC leo Bunju

Muktasari:

  • Mbelgiji huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia Simba, leo ataanza kibarua chake akiwa na msaidizi wake Selemani Matola.

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Simba, Sven Vandenbroeck atakutana kwa mara ya kwanza na wachezaji wa Simba leo kwenye Uwanja wa Simba MO Arena, Bunju.

Mbelgiji huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia Simba, leo ataanza kibarua chake akiwa na msaidizi wake Selemani Matola.

Kocha Vandenbroeck atakutana na benchi la ufundi la Simba katika kambi ya timu hiyo iliyopo Mbweni na watapata chakula cha mchana kwa pamoja na baada ya hapo wataanza safari ya kwenda mazoezini kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena.

Baada ya kufika katika uwanja huo wa mazoezi wa Simba, Vandenbroeck ndio atakutana na wachezaji wote waliokuwepo katika kikosi hiko ukiondoa wale waliokuwa katika majukumu ya timu ya taifa ya Kilimanjaro Stars.

Vandenbroeck amekuja kuchukua nafasi ya Mbelgiji mwenzake Patrick Aussems aliyeondoka baada ya uongozi wa Simba kukatisha naye mkataba kwa madai ya kushindwa kuzisimamia ikiwemo masuala ya kinidhamu ndani ya timu.