Kocha Taifa Stars apewa mchongo kuiua Uganda

Muktasari:

  • Akizungumza Dar es Salaam jana, Chambua alisema hakuna timu dhaifu katika mashindano, hivyo ameitaka Taifa Stars kufanya maandalizi ya kutosha kujiandaa kwa mchezo huo.

Dar es Salaam. Wakati kocha wa timu ya Taifa ya Uganda, ‘The Cranes’, Sebastien Desabre akishutumiwa kwa madai ya kuteua kikosi dhaifu, baadhi ya wadau wamesema Taifa Stars haipaswi kudharau mchezo huo.

Baadhi ya mashabiki Uganda wamedai Desabre ameteua kikosi ambacho kina uwezekano mkubwa wa kufungwa dhidi ya Taifa Stars, katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), Jumapili wiki hii.

Baadhi ya vyombo vya habari Uganda vimetoa maoni tofauti baada ya Desabre kuwaita wachezaji wawili wasiokuwa na timu Geofrey Walusimbi na Hassani Waswa na kuwatema baadhi ya nyota.

Pamoja na Desabre kutetea uteuzi wake, nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema uteuzi wa kocha huyo raia wa Ufaransa ni mtego kwa Taifa Stars.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Chambua alisema hakuna timu dhaifu katika mashindano, hivyo ameitaka Taifa Stars kufanya maandalizi ya kutosha kujiandaa kwa mchezo huo.

Chambua alisema kila mchezaji anatakiwa kuwajibika ipasavyo kwa nafasi yake kwa kufuata vyema maelekezo ya benchi la ufundi.

Pia alisema kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike anatakiwa kuwaandaa wachezaji kisaikolojia kwa kuwaamisha kuwa mechi hiyo ni ngumu.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars Mussa Hassani ‘Mgosi’ alisema wachezaji wanapaswa kujitambua kwa kuamini kuwa ni mchezo mgumu uliobeba matumaini ya Watanzania.

Akizungumza jana, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema wameandaa utaratibu wa kutoa hamasa kwa Taifa Stars ili kupata ushindi dhidi ya Uganda. “Siwezi kusema tumeandaa nini, lakini utaratibu mzuri tulioandaa kwa vijana wetu utasaidia wachezaji kujituma,” alisema Karia.

Wachezaji wanaocheza soka la kulipwa waliofanya mazoezi jana asubuhi ni Simon Msuva Difaa El Jadida ya Morocco, Rashid Mandawa (BDF/ Botswana), Himid Mao (Petrojet/ Misri), Shiza Kichuya (Enppi/ Misri), Yahya Zaid (Ismailia/ Misri), Hassan Kessy (Nkana/ Zambia) na Thomas Ulimwengu (JS Saoura/ Algeria).

Wachezaji wa ndani walikuwa Aishi Manula, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Ally Mtoni, Kenned Juma, Erasto Nyoni, Feisal Salum, Mudathir Yahya, Metacha Mnata, Aaron Kalambo, John Bocco, Suleman Salula na Vincent Phillip.