Kocha Yanga atupiwa virago Zambia

Muktasari:

  • Mwandila alijiunga na Yanga mwaka 2018 akihudumu katika nafasi ya kocha wa viungo na baadaye kocha msaidizi chini ya makocha George Lwandamina na Mwinyi Zahera

Dar es Salaam. Klabu ya Buildcon imevunja mkataba wake na aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila kwa makubaliano ya pande mbili.

Mkataba baina ya Mwadila na Buildcon ulivunjika rasmi juzi, Februari 17 kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo kwenda kwa kocha huyo.

“Buildcon Football Club na Noel Mwandila anayehudumu nafasi ya kocha msaidizi leo Februari 17, tumefikia makubaliano ya kuvunja mkataba,” ilifafanua sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Hector Mulindwa.

 Mwandila anaachana na klabu hiyo ikiwa ni miezi miwili tu tangu alipojiunga nayo akitokea Yanga ambayo aliachana nayo baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuitumikia kwa miaka miwili.

Hata hivyo licha ya barua hiyo kuonyesha kuwa pande hizo mbili zimevunja mkataba kwa makubaliano binafsi, nyuma ya pazia inaonekana imechochewa na kufanya vibaya kwa timu hiyo katika mechi zake za hivi karibuni za Ligi Kuu ya Zambia ikiwa chini ya Mwandila ambaye kabla ya kujikita na ukocha alikuwa winga machachali wa klabu ya Green Buffaloes na timu ya Taifa ya Zambia.

 Buildcon haijapata ushindi katika michezo mitano mfululizo iliyocheza hivi karibuni ikifungwa minne na kutoka sare mmoja na ipo katika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi  25.