Kocha afichua kisa cha nyota Coastal Union kuanguka

Muktasari:

  • Mgunda alisema ratiba za mechi za mchana zipo kwenye utaratibu lakini ameiomba TFF kuangalia kwa umakini kwani iko siku atakuja kufa mchezaji uwanjani kwani wamekuwa wakicheza soka kwa mateso makubwa.

MWANZA. KOCHA wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema iko haja ya Shirikisho la Soka  Tanzania (TFF), kuangalia upya ratiba za mechi za mchana za Ligi Kuu kwa kuwa iko siku  atakuja kufa mtu  uwanjani kwani wachezaji wamekuwa wakipata tabu kwani wanacheza katika mazingira ya joto na jua kali.

Jumatatu ya wiki hii beki wa kushoto wa Coastal Union Adeyum Salehe alidondoka ghafla wakati wa mchezo wao na Mbao FC  huku sababu kubwa ikilezwa kukosa maji mwilini kutokana na jua na joto kali katika mchezo huo uliopigwa saa 8 mchana.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mgunda alisema katika jambo ambalo linawapa mateso wachezaji ni kucheza mechi mchana kwani wamekuwa wakiteseka sana kutokana na hali ya sasa ya hewa kuwa na joto kali linaloambatana na jua.

Mgunda alisema ratiba za mechi za mchana zipo kwenye utaratibu lakini ameiomba TFF kuangalia kwa umakini kwani iko siku atakuja kufa mchezaji uwanjani kwani wamekuwa wakicheza soka kwa mateso makubwa.

“Niseme jambo wachezaji wanapata mateso makubwa sana kucheza mechi za mchana haswa kipindi hichi cha jua na joto kali nasema iko siku yatatokea maafa uwanjani niombe hili liangaliwe upya najua michezo inachezwa kwa ajili ya kurusha kwenye runinga lakini hali ni mbaya sana,”alisema Mgunda.

Hata hivyo Daktari  wa timu ya Coastal Union, Kitambi Mganga alisema kuna madhara makubwa sana kwa mchezaji kucheza mechi kipindi cha jua na joto kali kwani kunafanya apungukiwe maji mwilini na ndilo tatizo lililomtokea mchezaji Adeyum Salehe.

“Ni hatari sana kucheza mchana haswa kipindi cha jua kali kama hili kunaweza kusababisha kifo kwa mchezaji kwani anaweza kufanya moyo kusimama (Heart attack),” alisema Mganga.

Kwa upande wake Adeyum Salehe alisema licha ya kucheza mechi hizo mchana lakini wamekuwa wakipata mateso makubwa haswa jua likiwa kali.

Hata hivyo mechi hizo zimekuwa zikipangwa ratiba za mchana ili kuweza kurushwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV.