Kocha wa Namungo: Nyie Yanga tusijuane kesho!

Muktasari:

Kocha wa Namungo FC amesema kesho ni mpira tu na hakuna kujuana, kikubwa ni kutengeneza heshima

Kocha wa Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi, Bakari Malima amesema kesho Jumapili ni mpira tu na hakuna kujuana kwenye kombe la FA.

Malima amedai hataki kujuana na klabu ya Yanga FC awapo kazini kwani anapenda mkate wake unaopatikana katika bakery ya Namungo.

Si hivyo tu, kocha huyo ameendelea kujitapa kwamba anataka kujenga heshima kwa kuhakikisha anapandisha timu hiyo na kushiriki ligi kuu.

Majigambo hayo yamekuja baada ya kukumbushiwa na mwandishi kwamba kesho wachezaji wake wanakwenda kuchuana na tumu yake aliyoichezea miaka ya tisini.

“Kesho ni mpira hakuna kujuana kwenye kombe la FA, ujue kitu cha kwanza hapa niko kazini , lazima nitengeneze mazingira ya heshima kutoa timu ilipo kwenda juu na mimi nitengeneze CV yangu, mkate wangu naupata hapa Namungo,”amesema Malima

Amesema alichezea Yanga miaka hiyo na kwa mafanikio ila sasa ni kocha na anahitaji mafanikio katika nafasi ya ukocha.

“Sasa mapenzi yangu na kazi yang ni Namungo ili ifanye vizuri..kule (Yanga) nilicheza sawa kwa wakati huo kwa mafanikio ila sasa ni kocha nahitaji mafanikio kwenye ukocha kwa kuitoa Namungo hapa ilipo kupeleka juu,”amesema Malima

Toka kuanza kwa michuano hiyo Namungo FC inaongoza ikiwa imecheza mara  14 bila kufungwa.Yaani wao ni sare na kushinda tu.