Kwa Yanga hii kufuzu tumwachie Mungu

Thursday July 19 2018

 

Dar es Salaam. Kipigo cha mabao 4-0 ilichokipata Yanga jana kutoka kwa Gor Mahia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kimegeuka gumzo huku wakongwe wa soka nchini wakieleza nafasi ya Yanga kufuzu robo fainali inategemea muujiza.

Yanga inakamata mkia katika Kundi D ikiwa na pointi moja huku USM Algiers ya Algeria ikiwa kinara wa kundi hilo na pointi saba wakati Gor Mahia yenyewe ni pili ikiwa na pointi 5 na Rayon Sports iko kwenye nafasi ya tatu na pointi mbili.

Yanga imebakiza mechi tatu za marudiano ambapo itacheza na Gor Mahia Dar es Salaam itawafuata Rayon nchini Rwanda na kumaliza mechi za makundi nyumbani dhidi ya USM Algiers.

Wakongwe wa soka nchini wamezitazama mechi hizo na kueleza kuwa nafasi ya Yanga kushinda na kufuzu hatua ya robo fainali inasubiri muujiza pekee.

Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Iddi Pazi alisema kama siyo adhabu angeishauri Yanga ijitoe kwenye mashindano hayo ijipange upya kwa ajili ya Ligi Kuu.

"Gor Mahia haikuwa timu ya kuifunga Yanga mabao 4-0, lakini yote hayo yanasababishwa na matatizo ya klabu ambayo yamewaathiri hadi wachezaji, kama wasipochukua hatua mapema hata kwenye ligi msimu huu mambo yatakwenda ndivyo sivyo," alisema Pazi.

Nyota wa zamani wa Yanga, Abed Mziba alisema timu yao kutinga robo fainali labda yatokee maajabu kinyume na hapo wanasubiri kuhitimisha ratiba tu.

"Wachezaji wamekata tamaa, mechi ya jana ni kama walikwenda kutimiza wajibu tu, lakini sio kushindana, Yanga sasa ina matatizo makubwa kuna wachezaji pale hawana mchango kwenye timu, tunawajua lakini wapo tu, hatuwezi kuendelea," alisema Mziba.

Winga wa Simba, Dua Said alisema kufungwa mabao 4-0 hakumaanishi wachezaji wa Yanga ni wabovu kupitiliza, lakini wachezaji hawako sawa kisaikolojia.

"Wachezaji nao wamejitwika matatizo yanayoendelea klabuni, kwa hali hiyo watapata tabu sana, walipaswa waonyeshe jitihada binafsi kwani wanapofanya vizuri uwanjani pesa itapatikana tu hata kama ni ndogo, lakini hicho kinachoendelea ndiyo kinawamaliza zaidi," alisema Dua.

Advertisement