Kwa Yanga hii mtakoma tu!

Muktasari:

  • Zahera alisema akimalizana na taji hilo, wanachama na mashabiki wa Yanga wajiandae kulishuhudia taji la Kombe la FA likitua Jangwani sambamba na lile la Ligi Kuu Bara mataji waliyoyatema kwa watani wao wa Simba kwa misimu tofauti.

CHAMA la Wana limemtibua Kocha Mwinyi Zahera baada ya wikiendi iliyopita kuwanyoosha vijana wake wa Yanga kwa bao 1-0 na kuvunja rekodi yao ya ubabe katika Ligi Kuu Bara ambapo kabla ya hapo ilikuwa haijaonja kipigo chochote.

Sasa unaambiwa kipigo hicho kimempa mzuka Zahera na kula kiapo kwa mashabiki wake kuwa, watulie kwani atakachokifanya kwa wapinzani wake kuanzia sasa watajuta kumfahamu.

Kocha huyo Mkongo akaenda mbali na kuwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa kuna zawadi tatu alizowaandalia kwa sasa ili kuwafuta machungu, akianza na taji la Kombe la SportPesa Super Cup 2019 linaloanza leo Jumanne, huku yeye akianza dhidi ya Kariobang Sharks ya Kenya.

Zahera alisema akimalizana na taji hilo, wanachama na mashabiki wa Yanga wajiandae kulishuhudia taji la Kombe la FA likitua Jangwani sambamba na lile la Ligi Kuu Bara mataji waliyoyatema kwa watani wao wa Simba kwa misimu tofauti.

Yanga ndio ilikuwa wa kwanza kubeba Kombe la FA baada ya michuano hiyo kurudishwa 2015-2016 tangu ilipozimika mwaka 2002, lakini msimu uliofuata wa 2016-2017 Simba iliwanyang’anya na wao kulitema msimu uliopita na kubebwa na Mtibwa Sugar.

Katika Ligi kuu Bara Yanga ilikuwa inalishikilia taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo, lakini Simba ililinyakua msimu uliopita kitu ambacho Zahera alisema wapinzani wake katika michuano yote mitatu anayoshiriki wajiandae kwani sasa ndio watamkoma.

Jumamosi iliyopita wakiwa mjini Shinyanga, Zahera na vijana wake walipoteza mchezo mbele ya Chama la Wana naye amefichua Yanga kama timu kubwa inapaswa kumaliza msimu ikiwa na idadi kubwa ya vikombe, hivyo atahakikisha mataji hayo matatu yanatua Jangwani.

Ikiwa inaongoza Ligi Kuu huku ikifuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, Zahera anaamini Yanga ni lazima itwae makombe hayo mawili pamoja na lile la SportPesa ambalo leo inafungua dimba dhidi ya Sharks.

Zahera alisema anayapa uzito mkubwa mashindano ya SportPesa Super Cup na atatumia kikosi kamili tofauti na alivyofanya kwenye Kombe la Mapinduzi 2019 ambako alipeleka kundi kubwa la wachezaji wa kikosi cha vijana.

“Timu yoyote inapoanza msimu wa ligi inapaswa kuwa na malengo iliyojiwekea. Sisi Yanga msimu huu tulipanga malengo matatu ambayo ni kutwaa ubingwa wa ligi, Kombe la Azam Federation Cup (FA) na hili la SportPesa, hivyo nitapanga kikosi kamili kesho (leo).

Nimewaambia wachezaji wangu tunahitajika angalau kucheza mechi tatu kwenye haya mashindano ya SportPesa ambayo naamini ni sehemu ya kuwafurahisha Wanayanga,” alisema Zahera.

Kauli hiyo ya Zahera, imeungwa na nahodha Ibrahim Ajibu ambaye amedai awamu hii hawako tayari kuona Kombe la SportPesa linakwenda nje ya ardhi ya Tanzania.

“Awamu mbili tulizoshiriki hapo nyuma hatukufanya vizuri kwa sababu tulikuwa tunacheza bila ya kuwa na kikosi kamili lakini kwa sasa ni tofauti kidogo kwa sababu tunacheza tukiwa tumekamilika pia tuna kocha mpya,” alisema Ajibu kinara wa asisti katika Ligi Kuu akiasisti 15 na kufunga mabao sita mpaka sasa.

Kwa upande wa Kariobangi Sharks, Kocha Msaidizi Collins Omondi alisema wako tayari kupambana na Yanga kwenye mechi ya leo na hawatishwi na ukubwa wa jina lake.

“Tunafahamu Yanga ni timu kubwa hapa na ina mashabiki wengi lakini mwisho wa siku ndani ya uwanja wanachezaji wachezaji 22 ambapo kila upande unakuwa na wachezaji 11.

Tumejiandaa vizuri kukabiliana nao na tunaamini uzoefu tulioupata kwenye mechi za kimataifa msimu huu utatusaidia,” alisema Omondi.

Mechi nyingine leo itakuwa ni baina ya Singida United itakayocheza na Bandari FC wakati kesho kutakuwa na mechi baina ya Mbao FC dhidi ya Gor Mahia huku Simba ikicheza na AFC Leopards.

Michuano ya SportPesa ilianzishwa mwaka 2017 ikifanyika jijini Dar es Salaam na Gor Mahia kubeba taji kwa kuwafunga mashemeji zao wa AFC Leopards kwa mabao 3-0 na kupata tiketi ya kuvaaa na Everton katika mechi iliyooishwa kwa Wakenya hao kulala 2-1 Uwanja wa Taifa.

Msimu uliopita ikiwa ni michuano ya pili, Gor Mahia ilibeba tena taji hilo kwa kuicharaza Simba mabao 2-0 katika fainali iliyopigwa mjini Nakuru, Kenya na kusafiri hadi England kuvaana na Everton ya Ligi Kuu England (EPL) na kufumuliwa mabao 4-0.

Na msimu wa mwaka huu mbali na zawadi ya fedha kombe na medali kwa mshindi pia itapata nafasi ya kuvaana na Everton watakaokuja nchini kwa mara ya pili.