Kwasi wa Simba amfuata Makambo Guinea

Muktasari:

  • Beki Asante Kwasi mbali na kukutana na Heritier Makambo pia amekutana na kocha wake wa zamani wa Simba.

Dar es Salaam. Beki wa zamani wa Simba, Mghana Asante Kwasi amekamilisha usajili wa kujiunga na Hafia FC ya jijini Konakry, Guinea.
Kukamilika kwa usajili huo sasa kutamfanya Kwasi kupata nafasi ya kukutana na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo anayechezea Horoya.
Makambo kwa sasa anaitumikia Horoya AC mabingwa watetezi wa ligi nchini humo ambao pia walimsajili Mghana mwingine Enock Atta na kiungo Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu wote kutoka Azam.
Akiwa Hafia, Kwasi amepata nafasi ya kukutana na kocha wake wa zamani wa viungo Aimen Habib ambaye naye yuko katika benchi la timu hiyo.
Habib aliwahi kufanya kazi Simba akimsaidia kocha Mfaransa Pierre Lechantre ambapo Kwasi alikuwa beki aliyekubalika kwa makocha hao mbele ya nahodha msaidizi wa Simba Mohammed Hussein 'Tshabalala'.
Simba ililazimika kuachanana na Kwasi mwisho wa msimu uliopita kutokana na kutumia muda mwingi akiwa majeruhi na kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza iliyorejea kwa Tshabalala.