LIGI KUU BARA: Yanga yang’ara, Azam yashikwa

Friday February 20 2015

Kiungo wa Yanga, Andry Coutinho (kulia) na

Kiungo wa Yanga, Andry Coutinho (kulia) na Amissi Tambwe wakishangilia baada ya kufunga bao la pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Yanga ilishinda mabao 3-0. Picha na Godfrey Kahango. 

By Julius Kihampa na Dorice Maliyaga, Mwananchi

Mbeya/ Pwani. Baada ya miaka sita Yanga imepata ushindi  wa kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya  kwa kuichakaza Prisons mabao 3-0 wakati  Azam ikilazimishwa sare ya 0-0 na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Ushindi huo unaifanya Yanga ikalie usukani wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 28, wakati mabingwa watetezi, Azam wakishuka nafasi ya pili na pointi 26.

Kiungo Andrey Coutinho alikuwa shujaa baada ya kufunga bao moja na kutengeneza mawili yaliyofungwa na kinara wa ufungaji Yanga, Simon Msuva.

Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi na kuonekana kupania ushindi dhidi ya wachovu Prisons na kufanikiwa kufunga mabao mawili ndani ya dakika 11 za kipindi cha kwanza.

Msuva alifunga bao la kwanza dakika ya 4, akiunganisha mpira wa kona wa Coutinho.

Kuingia kwa bao hilo  kuliwafanya wachezaji wa Prisons na benchi lao la ufundi kumlalamikia mwamuzi Zakaria Jacob kwa madai kuwa Msuva alifanya makosa kwa kumgonga kipa wao, Mohamed Yusuph kabla ya kufunga bao hilo.

Baada ya vurumai hizo Prisons walirejea na kufanya mashambulizi kadhaa na kupoteza nafasi za kufunga mabao dakika ya 9 na 10 kupitia kwa Jeremiah Juma na Jacob Mwakalobo baada ya mashuti yao kutoka nje.

Dakika  ya 11 Yanga waliandika bao la pili kupitia kwa Coutinho baada ya shuti lake kumchanganya beki wa Prisons, Lugano Mwangama na kujikuta akiusindikiza wavuni badala ya kuokoa.

Kipindi cha pili Yanga iliongeza bao la tatu kupitia kwa Msuva akiunganisha kona safi iliyochongwa na Coutinho.

Kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi,  pamoja na kuichapa El Merreikh mwishoni mwa wiki mabao 2-0, safu ya ushambuliaji wa Azam jana ilishindwa kuipenya ngome ya Ruvu Shooting na kulazimishwa sare ya 0-0.

Azam walijaribu kufunga dakika ya 26 kupitia kwa Kipre Tchetche,  lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango kabla ya Ruvu Shooting kujibu mashambulizi dakika ya 36 kupitia kwa Yahaya Tumbo, lakini shuti lake lililokolewa kistadi na kipa Aishi Manula.

Azam itacheza na Prisons wakati Mbeya City itaivaa Yanga Jumapili.

Advertisement