Lampard kuwatupia virago nyota nane Chelsea

London, England. Frank Lampard anajianda kuisafisha Chelsea kwa kuwaonyesha mlango wa kutokea wachezaji nane kwa mujibu wa The Sun.

Kipa Kepa Arrizabalaga ameshindwa kuonyesha ubora wake msimu huu na kupoteza nafasi kwa kipa Willy Caballero, ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa watatimuliwa na Lampard.

Viungo Ross Barkley na Jorginho pia wanaweza kuachwa pamoja na beki wa kushoto Marcos Alonso na Emerson, wakati Kurt Zouma, Willian na Pedro watakuwa wakiangaliwa mwenendo wao kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu.

Hiyo imekuja baada ya kikosi cha Lampard kupokea kipigo cha mabao 3-0 katika Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora nyumbani na Bayern Munich, huku pia ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England.

Kipigo hicho kikubwa kwa Lampard kimeonyesha jinsi kikosi chake kinavyoitaji mabadiliko kabla ya kuanza kufikiria ubingwa.

Lampard tayari ameshatumia pauni 37milioni kumsajili winga Hakim Ziech kutoka Ajax, ambaye atajiunga na klabu hiyo mwisho wa msimu.

Inaonekana bado anataka kusajili wengine wanne wakiwamo beki wa kushoto Ben Chilwell kutoka Leicester na kipa wa Atletico Madrid, Jan Oblak.