VIDEO: Ligi Kuu Tanzania yapigwa ‘STOP’ kwa mwezi mmoja, kisa Corona

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Michezo yote inayokusanya watu wengine imesimamishwa kwa siku 30 kuanzia leo Jumanne Machi 17 kwa ajili ya kuendelea kuchukua tahadhari zaidi ya Virusi vya corona.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametangaza kusimamishwa kwa shughuli zote za kimichezo zinazokusanya watu wengi ikiwamo Ligi kuu Tanzania bara kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona vinavyosambaa kwa kasi duniani.


Waziri mkuu ametangaza hayo leo Jumanne Machi 17, 2020 wakati akitangaza uamuzi wa serikali juu ya hatua zinazochukuliwa kujikinga na Ugonjwa wa Corona.
“Tumesitisha michezo yoye inayokusanya makundi ya watu, kama vile Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ligi daraja la pili, Ligi daraja la kwanza, michezo ya shule za msingi, michezo ya shule za sekondari pamoja na ile ya mashirika ya umma ambayo inapangwa kila mwaka yote imesitishwa kwa muda wa mwezi mmoja” amesema Majaliwa


Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka Wizara ya Habari, sanaa utamaduni na Michezo kuyaandikia mashirikisho ya michezo nchini kusitisha michezo hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja.


Hatua hii inakuja ikiwa tayari Tanzania kupitia kwa Waziri wa afya kutangaza kuwapo kwa mgonjwa mmoja wa Corona kaskazini mwa Tanzania akiendelea na matibabu.