Ligi Kuu yaweka rekodi ya mabao

Friday May 31 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.Wakati pazia la Ligi Kuu msimu wa 2018/2019 likifungwa rasmi wiki hii, mabao yaliyofungwa yamesababisha kuwekwa rekodi tofauti ambazo hapo kabla hazikuwahi kushuhudiwa katika ligi hiyo.

Msimu huo umeweka rekodi ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya mabao ya kufungwa kuliko msimu mwingine wowote ule katika ligi hiyo ambayo msimu uliopita ilishirikisha timu 20.

Jumla ya mabao 744 yalifungwa msimu uliomalizika, huku timu nne zilizomaliza katika nafasi ya juu zikichangia mabao 227 ambayo ni zaidi ya robo ya mabao yote yaliyofungwa. Simba iliyotwaa ubingwa imefunga mabao 77, Yanga (56), Azam (54) na KMC (40).

Hakuna timu ndani ya miaka 19 ya Ligi Kuu iliyomaliza msimu mmoja ikiwa imevuna pointi 93 ambazo msimu huu zimewekwa na Simba.

Katika hali ya kushangaza, licha ya nyota mbalimbali wa ligi hiyo kuwa wamehusika katika kupatikana mabao 744, bado wachezaji hao wameendelea kuteswa na rekodi iliyowekwa mwaka 1999 na mshambuliaji wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

Mmachinga aliibuka mfungaji bora akiwa amepachika mabao 26, kwani mfungaji bora wa msimu uliomalizika ni Meddie Kagere wa Simba ambaye amefumania nyavu mara 23.

Advertisement

Msimu 2017/2018 ambao Simba ilitwaa ubingwa wa 19 wa Ligi Kuu yalifungwa mabao 470, aliyeibuka mfungaji bora alikuwa Emmanuel Okwi akipachika mabao 20.

Na msimu 2016/2017 yalifungwa mabao 474, Saimon Msuva aliyekuwa Yanga na Abdulraham Mussa wa JKT Tanzania, waligawana tuzo ya ufungaji bora kutokana na kila mmoja kufunga mabao 14.

Msimu 2015/2016 ambao timu ziliongezeka kutoka 14 hadi 16, mabao yaliyofungwa yalikuwa 495, ina maana kadri misimu ilivyokuwa inasogea mbele ndivyo idadi ya mabao ilikuwa ikipungua.

Aliyeibuka kinara wa mabao kwenye msimu huo ambao Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo kabla ya kuchukua la tatu, alikuwa Amissi Tambwe akiwa na mabao 21.

Mara ya kwanza Msuva kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ilikuwa msimu 2014/2015 ambapo alifunga mabao 17 na kuisaidia Yanga kutwaa ubingwa huku yakifungwa jumla ya mabao 348.

Msimu ambao Azam ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza 2013/2014 yalifungwa mabao 407 na aliyeibuka kinara wa mabao alikuwa Tambwe kipindi hicho akiitumikia Simba alipofunga mabao 19.

Msimu mmoja nyuma 2012/2013 kabla ya kutwaa ubingwa Azam ilikuwa miongoni mwa timu ambazo zilikuwa katika nafasi ya kutwaa ubingwa huo ikiwa na Kipre Tchetche ilimaliza katika nafasi ya pili, nyuma ya Yanga iliyotwaa ubingwa huo. Katika msimu huo yalifungwa mabao 369 na aliyeibuka kuwa mfungaji bora alikuwa Tcheche ambaye aliifungia Azam mabao 17 kati ya 46 waliyopata.

Awamu nyingine ambazo ilitwaa tuzo hiyo ambapo unaweza kusema ni ‘hat trick’ ya tuzo za ufungaji bora kwa Azam ilikuwa misimu miwili nyuma ambapo alitwaa John Bocco akiwa na mabao 19 kwenye msimu 2011/12.

Ndani ya msimu huo ambao Simba ilichukua ubingwa huku Azam ikishika nafasi ya pili, yalifungwa jumla ya mabao 412, Simba (47), Azam (40) na Yanga (41) ikichangia kwa pamoja mabao 128.

Mrisho Ngassa kipindi hicho akiichezea Azam alikuwa mchezaji wa kwanza kutoka kwenye timu hiyo kuchukua tuzo ya ufungaji bora wa Ligi Kuu kwa mabao 18, msimu 2010/2011 jumla ya mabao 274 yalifungwa.

Katika msimu 2009/2010, tuzo ya ufungaji bora wa Ligi Kuu ilienda kwa mshambuliaji aliyekuwa akiitumikia Simba, Mussa Hassani ‘Mgosi’ kwa mabao 18 huku ndani ya msimu huo yakifungwa mabao 307.

Kwa ujumla ndani ya misimu 10 ya Ligi Kuu tangu mwaka 2009/2010 hadi 2018/2019 yamefungwa jumla ya mabao 4,300.

Katika idadi hiyo ya mabao Simba imefunga 488 na wamechangia asilimia 11. Yanga ni 505 ikiwa ni asilimia 11.7 huku upande wa Azam ni 416 ikiwa ni sawa na asilimia 9.6.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na KMC, Elias Maguli alisema idadi kubwa ya mabao yaliyofungwa yamechangiwa na ongezeko la timu.

“Zamani ligi ilikuwa na timu 14 safari hii ni 20, katika uhalisia wa kawaida utaona kwamba ni lazima idadi ya mabao iongezeke,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Taifa Stars.

Advertisement