Liverpool, Arsenal zagawa dozi kwa Chelsea, Aston Villa

Muktasari:

Kikosi hicho kinachonolewa na Ole Gunnar Solskjaer leo Jumapili kilitia aibu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa West Ham United, shukrani kwa mabao ya kila kipindi Andriy Yarmolenko, aliyefunga kipindi cha kwanza na Aaron Cresswell, aliyeweka kwenye kamba kwa friikiki dakika sita kabla ya mechi kumalizika.

London, England. Liverpool imeendelea kuongoza Ligi Kuu kwa tofauti pointi tano kwa Manchester City baada ya kuifunga Chelsea kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Arsenal imerudi katika nne bao baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa, huku West Ham ikipanda hadi nafasi ya tano baada ya kuichapa Manchester United kwa mabao 2-0.

Vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool ilikuwa ya kwanza kupata mabao yake kupitia kwa Trent Alexander-Arnold kwa mpira wa adhabu kabla ya Roberto Firmino kufunga bao la pili kwa kichwa.

Chelsea ilipata bao la kusawazisha kupitia Cesar Azpilicueta, lakini VAR ilikataa bao hilo ikidai mfungaji alikuwa ameotea, hata hivyo kiungo N’golo Kante alifunga bao la kufutia machozi kwa wenyeji katika dakika 71.

Kwenye Uwanja wa Emirates, bao la mkwaju wa adhabu la mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang lilitosha kuwapa ushindi wachezaji 10 wa Arsenal waliotoka nyuma na kuichapa Aston Villa.

Aubameyang amefunga bao lake la saba msimu huu na kuihakikisha Gunners pointi tatu muhimu baada ya kucheza kwa dakika pungufu kuanzia dakika 41, baada ya insley Maitland-Niles kupewa kadi nyekundu.

Katika mchezo huo mabao mengine ya Arsenal yalifungwa na Pépé kwa mkwaju wa penalti dakika 59 na Chambers katika dakika 81 wakati mabao ya Aston Villa yalifungwana McGinn (dakika 20), Wesley (dakika 60)

Awali Manchester United kila siku afadhali ya jana. Mechi sita walizocheza kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, tayari wamechapwa mara mbili, wameshinda mbili na sare mbili, jambo linalowafanya kuwa na pointi nane, zinazozidi kuweka mbali na timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kikosi hicho kinachonolewa na Ole Gunnar Solskjaer leo Jumapili kilitia aibu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa West Ham United, shukrani kwa mabao ya kila kipindi Andriy Yarmolenko, aliyefunga kipindi cha kwanza na Aaron Cresswell, aliyeweka kwenye kamba kwa friikiki dakika sita kabla ya mechi kumalizika. Baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Leicester City kisha 1-0 tena dhidi ya Astana, Man United walionekana kama wamerudi kwenye kasi yao ya ushindi sare ya Southampton na kipigo kutoka kwa Crystal Palace, mambo yalivurugika kwa kipigo hicho cha West Ham na kuonekana kama ugonjwa wao wanaumwa, bado hawajapona.

Katika mchezo huo wa jana, kocha Solskjaer aliendelea kuwakosa nyota wake kadhaa akiwamo Anthony Martial, Luke Shaw na Paul Pogba kutokana na kuwa majeruhi, kikosi chake hakikuwa na maajabu licha ya kukaa na mpira muda mwingi kuliko wapinzani wao. Man United ilipiga mashuti matatu golini bila ya kufunga, wakati wenzao walilenga goli mara mbili tu katika mashuti yao sita na kufunga mara mbili.

Mashabiki wa wababe hao wa Old Trafford wameanza kuwa na wasiwasi mkubwa na uwezo wa kikosi chao kwamba wanapoteza dhidi ya timu kama Crystal Palace na West Ham United, hali itakuwaje watakapokabiliana na vigogo kama Arsenal, Manchester City, Tottenham Hotspur na Liverpool.

Man United walishaitambia Chelsea kwenye mchezo wa kwanza walipowafunga 4-0 na kuleta matumaini mapya ndani ya msimu huu kabla ya mambo kutibuka na sasa wanatiririka tu kuondoka kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo. Kabla ya mechi za Arsenal na Chelsea, Man United walikuwa kwenye nafasi ya saba, hivyo ushindi wowote kwa wapinzani wake hao wa Big Six utakuwa umewaporomosha zaidi na kuwaweka mbali ya Top Four. Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Wolves waligomea kipigo cha pili mfululizo baada ya kusawazisha katika dakika za majeruhi kupata sare ya 1-1 mbele ya Crystal Palace huko Selhurst Park.

Katika mchezo huo, Leander Dendoncker  alijifunga mapema kabisa kwenye kipindi cha pili na kuwafanya Palace kuongoza, kabla ya Wolves kujikuta wakicheza pungufu kufuatia Romain Saiss kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa njano mbili. Wakati Palace wakiamini wanang'oa pointi zote tatu kwenye mchezo huo, Diogo Jota aliwarudisha Wolves mchezoni akifunga kwenye dakika za majeruhi. Ligi hiyo itarajiwa kuendelea kwa michezo mingine kadhaa, ambapo Arsenal walikuwa na shughuli ya kuwakabili Aston Villa huko Emirates na Chelsea walijimwaga Stamford Bridge kukipiga na vinara na mabingwa wa Ulaya, Liverpool.