Liverpool haikamatiki yaichapa Spurs ya Mourinho

Saturday January 11 2020

 

BAO la mshambuliaji wa Kibrazil, Roberto Firmino limetosha kuifanya Liverpool kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Tottenham, wakiwa ugenini.

Firmino alipachika bao hilo dakika ya 37 huku akimalizia pasi ya Mohamed Salah, ameifanya Liverpool kuendeleza rekodi yao tamu msimu huu ya kucheza michezo 21 ya Ligi Kuu England bila ya kupoteza.

Tottenham ipo chini ya kocha mwenye maneno mengi, Jose Mourinho, imeushindwa kuutafuna mfupa wa majogoo hao wa Anfield ambao kikosi chao kinanolewa na Jurgen Klopp ambaye kimeonekana kuwa bora tangu msimu uliopita.

Kama ilivyo kawaida ya Mourinho alitumia mbinu za kujilinda muda mwingi huku akishambulia kwa kushitukiza huku akikosa huduma ya mshambuliaji wake hatari Harry Kane ambaye anasumbuliwa na majeraha.

Lakini katika mchezo huo, alirejea Son Heung-Min ambaye alionyeshwa kadi nyekundu, Desemba 22 mwaka Jana katika mchezo dhidi ya Chelsea ambao walipoteza kwa mabao 2-0 baada ya kumchezea vibaya, Antonio Rudiger.

Ushindi kwa Liverpool umewafanya kuendelea kujikita katika kilele cha msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na pointi 61, wakifuatiwa na Leicester City wakiwa na pointi 45, Manchester City wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 44.

Advertisement


Advertisement