MO Dewji: Nitawapa Bodaboda wachezaji wote Simba

Muktasari:

Manchester United ni miongoni mwa klabu zimezoeleka kuweka kambi nchini Marekani wakijiandaa na msimu mpya.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi klabu ya Simba, Mohammed Dewji amehaidi kuwapa pikipiki aina Boxer yenye thamani ya Sh 2.4 milioni baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Dewji alisema hayo wakati wa kuipongeza timu hiyo kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo na zawadi hiyo imetoka kutoka kwake mwenyewe.

Alisema kuwa amewaomba wachezaji kutumia pikipiki hizo kama kitega uchumi na kuwapa ndugu zao ili kujiingizia kipato kila siku.

Alisema kuwa wanaweza kuingia mkataba na ndugu zao ambao hawana kazi na kujipatia sh 15,000 kwa siku mpaka hapo mkataba utakapo malizika.

“Nimefarijika kwa mafanikio ya timu ambayo yametokana na umoja wa ndani ya klabu baada ya kuanza mfumo mpya wa uongozi,” alisema Dewji.

Alisema kuwa zawadi hiyo itawajenga wachezaji na kuona tija kwa kazi waliyoifanya katika ligi kuu ya Tanzania Bara.

Mbali ya kuwapa Bodaboda, MO ameahidi kuipeleka timu hiyo Marekani au Ureno wakati wa kujiandaa kuanza kwa Ligi msimu ujao (Pre Season).

MO alisema wanataka kuhakikisha wanakuwa na maandalizi mazuri kwa timu yao ili kufanya vizuri katika mashindano wanayoshiriki msimu ujao.

"Mimi binafsi nilianza mazungumzo na baadhi ya watu nikiwa nchini marekani (Boston) na tayari tumefika sehemu nzuri hivyo Simba wataenda huko kujiandaa na Ligi," alisema.

Kwa umakini Mwekezaji huyo wa Simba, alisema ratiba hiyo itakuwa maalum baada ya mashindano ya Afcon ambayo yanatarajia kuanza mwanzoni mwa mwwzi wa sita.

"Kambi yetu itakuwa ni baada ya Afcon ndio vijana wataondoka kuelekea katika nchi mojawapo, hizi nchi hata klabu kubwa barani Ulaya nao wamekuwa wakienda wakati wa kujiandaa na Ligi," alisema.

Aliongeza msimu ujao watakuwa na kikosi kipana kwa kufanya usajili mkubwa huku wale wasiokuwa na mahitaji nao watawatoa kwa mkopo.