MO Dewji aweka wazi ujio wa mrithi wa Aussems Simba SC, awashukia wachezaji

Mwekezaji wa Simba na Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (Mo) 

Muktasari:

Licha ya kutotaka kuweka wazi anatoka katika nchi gani, Mo amesema kocha wao mpya ana kiwango cha kufundisha timu hiyo.

Dar es Salaam.Mwekezaji wa Simba na Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (Mo) amesema tayari wamempata kocha mpya wa timu hiyo atakayetambulishwa wiki hii.

Mo ametamka hayo kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo unaoendelea jijini Dar es Salaam.

Mo amesema tayari wamemalizana na kocha huyo mwenye kiwango cha kufundisha Simba.

Licha ya kutotaka kuweka wazi anatoka katika nchi gani, Mo amesema kocha wao mpya ana kiwango cha kufundisha timu hiyo.

Kocha huyo anaajiliwa baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Patrick Aussems kutupiwa virago hivi karibuni.

Awali, Mo alianza kuelezea mambo ambayo hakuridhishwa nayo wakati wa Aussems.

Alisema nidhamu ya baadhi ya wachezaji ilikuwa mbovu na ndicho chanzo cha kutimuliwa kwa kocha huyo.

Dewji alisema haridhishwi na mwenendo wa klabu hiyo huku akidai baadhi ya wachezaji hawana nidhamu.

"Niwambie wachezaji wote kwamba, Simba ni klabu kubwa, bodi haitomvumilia mchezaji asiyejua thamani ya Simba.

Alisema kuonyana onyana sasa imetosha, Simba inawalipa vizuri wachezaji na wao wanapaswa kulipa thamani ya kile ambacho klabu imewekeza.

Alisema hawataangalia jina la mchezaji, nidhamu kwanza na ndicho kimefanya wamemuondoa kocha wao, Aussems.

Mo alisema katika uongozi hakuna masihara akifafanua kwamba mbali ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu katika hatua za mwanzo, bado hajaridhishwa na mwenendo katika ligi ya nyumbani.

"Hata kama tunaongoza Ligi, Simba inapaswa icheze kama bingwa mtetezi, lakini si kwa kiwango cha sasa ambacho hakiniridhishi."