MO aifumua Simba

Friday August 16 2019

 

BODI ya klabu ya Simba chini ya Mwenyekiti, Mohammed Dewji umeanza kufanya mabadiliko ya kimfumo wa utawala ndani ya klabu hiyo baada ya kukamilisha mchakato wa kupata watumishi watano wa sekretarieti ya klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa kutoka ndani ya klabu hiyo, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo ambaye ataongoza Sekretarieti ya Simba, ni Senzo Mazingisa ambaye ni raia wa Afrika Kusini.
Mazingisa inaelezwa alishakuja Tanzania tangu jana kwa mazungumzo, ingawa viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wasiri juu ya hilo.
Mazingisa anarithi nafasi inayoachwa wazi na Crescentius Magori ambaye mkataba wake wa kuhudumu kwenye nafasi hiyo umemalizika.
Mbali na Mazingisa, mwandishi wa habari za michezo na mchambuzi wa soka wa kituo cha kuninga cha Azam TV ambaye zamani alikuwa mwandishi wa gazeti la Mwanaspoti, Gift Macha ndiye mkuu mpya wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo.
Mwingine ni Hashim Mbaga ambaye atakuwa na cheo kipya kilichoanzishwa na klabu hiyo, cheo cha meneja wa wanachama.
Nafasi nyingine ni ile ya ofisa meneja ambayo itaongozwa na Rehema Lucas wakati meneja wa habari upande wa mitandao ya kijamii na dijitali atakuwa ni Rabi Hume.

Advertisement