MO aingiza Simba vitani, Amwaga Ajira Kibao, Atoa Onyo Kali

Muktasari:

Ndio, Mo baada ya ukimya wa muda mrefu tangu alipotangazwa kuimiliki klabu hiyo kwa asilimia 49, jana Ijumaa amefunguka mambo mbalimbali huku akisisitiza adhma yake ya kuifanya Simba kuwa miongoni mwa klabu tano tishio Afrika.

KAMA bilionea na mwekezaji wa Simba Mohammed Dewji (MO), ametangaza vita na klabu tajiri barani Afrika akiahidi kuiwezesha klabu hiyo kuingia kwenye orodha ya timu tajiri nani anabaisha?

Ndio, Mo baada ya ukimya wa muda mrefu tangu alipotangazwa kuimiliki klabu hiyo kwa asilimia 49, jana Ijumaa amefunguka mambo mbalimbali huku akisisitiza adhma yake ya kuifanya Simba kuwa miongoni mwa klabu tano tishio Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, ameeleza harakati mbalimbali zinazoendelea ndani ya klabu hiyo kwa sasa zote zikiwa na lengo la kuleta mabadiliko makubwa.

Lakini, kama kuna jambo ambalo limewafurahisha mashabiki wa Simba basi ni kuongezwa kwa bajeti ya usajili, ambayo itaiwezesha Simba kushusha mastaa wa maana kikosini msimu ujao.

Mo amesema kuanzia msimu ujao, usajili wa Simba utalenga zaidi kwa wachezaji wenye uwezo mkubwa, wenye kujitoa na nidhamu.

“Wachezaji wote wasio na nidhamu basi wajiandae kuondoka Simba kwa sababu hatutawavumilia tena. Tunataka wale wenye uchungu, kujitoa na nidhamu ndiyo watabaki ndani ya klabu ya Simba na si vinginevyo.

“Hatutaki wachezaji wa majaribio ila tutasajili waliobora kwa ajili ya malengo yetu ya baadaye kwani, tulikuwa na malengo ya awali ambayo ni kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, malengo ya kati na ya muda mrefu, hivyo tunaendelea kujenga timu,” alisema MO.

Kuhusu usajili wa straika wa Ndanda FC, Vitalis Mayanga imeelezwa kwamba, Aussems alihitaji mbadala wa Shiza Kichuya kwa haraka, ambaye ni mzawa ndiyo sababu ya kusajili.

Hata hivyo, wakati Simba ikitangaza kusaka wachezaji wa kuongeza kwa ajili ya michuano ya kimataifa, aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdalah (Try Again), alisema kwa sasa Simba itasajili mchezaji ambaye yuko kwenye timu ya Taifa ya nchi yake, tofauti na hapo hakuna nafasi.

Bejeti kupanda

Mo alisema ili ufanye vizuri kimataifa ni lazima wawe wamejipanga kikamilifu kama ilivyo kwa timu pinzani, akitolea mfano Al Ahly ambao iliwachapa mabao bao 5-0 wiki iliyopita na itakutana tena kwenye mechi ya marudiano Jumanne jijini Dar es Salaam

“Kwanza, wote tuliumia kufungwa mara mbili mfululizo lakini ni mambo yanayotokea katika soka na ili ufanye makubwa ni lazima uwe na bajeti kubwa na maandalizi ya muda mrefu.

“Tunakoelea ni kupandisha bajeti ili tufikie malengo yetu ambayo ni kutwaa ubingwa wa Afrika.

“Huwezi kuwa na bajeti kama ya sasa halafu ufikie malengo yako wakati wenzetu wanasajili wachezaji kwa mabilioni ya fedha hivyo, hata sisi tutalazimika kununua wachezaji wa aina hiyo,” alisema Mo Dewji

Simba yaendeshwa kwa hasara

Mo Dewji ameeleza kwamba, “Tangu tuingie kwenye mfumo huu mpya tumekuwa tukijiendesha kwa hasara, hakuna faida tunayoingiza na kwenye biashara ni lazima ukubali hasara kwanza. Baadaye tutapata faida na hapo tutaendelea kufanya uwekezaji mkubwa baada ya kuimarisha kila kitu,”

Pia, alisema tayari mchakato wa kuibadili Simba kuwa kampuni umekamilika baada ya kupata usajili rasmi.

“Kusajili kampuni ya Simba tayari tumemaliza, zoezi linalofuata ni kutangaza ajira katika vitengo vyote, hivyo mwenye sifa ataomba na kufanyiwa usaili kwa vigezo vitakavyowekwa.

“kwenye hili tutakuwa makini kupata watu sahihi kwani hii ni kazi na ni kampuni kubwa,” alisisitiza Mo.

Uwanja Boko wakwama

Februari 15, mwaka huu, Simba ilikuwa ikabidhiwe uwanja wao wa mazoezi huko Bunju, lakini haitakuwa hivyo baada ya nyasi zao kuendelea kuzuiwa bandarini.

“Kuna vitu vya kiserikali vimekwamisha ila kila kitu hatua ya awali kipo tayari, tunasubiri serikali tu sasa ili tumalizie na hapo tutaendelea,” aliongeza.

Hata hivyo, habari ambazo Mwanaspoti limezipata ni kuwa nyasi hizo zimezuiwa kama kilelezo cha kesi ya viongozi wa zamani wa Simba inayoendelea mahakamani.

Kuiona Simba

2,000 tu

Unakumbuka lile nyomi la watu lililoujaza Uwanja wa Taifa wakati wa mechi ya Nkana ama JS Saoura? Basi Mo Dewji anataka kuona nyomi kama hilo ili kuwapa mzuka wachezaji na kuwamaliza Waarabu fasta tu. Yaani Mo anataka uwanja mzima ujae na shangwe zianze mwanzo mwisho na hapo kama Simba isipopata ushindi basi kuna mkono wa mtu aisee.

“Tumepunguza viingilio siku ya mechi na Al Ahly ili mashabiki waje kwa wingi uwanjani. Kiingilio kwa jukwaa la mzunguko ni 2000 tu. Tunahitaji sapoti yao sana na hapa tunaangalia ushindi na si kupata pesa za viingilio.

“Tunafahamu matokeo ya mwanzo hayakuwa mazuri na tuliumia wote lakini wasikate tamaa lolote linawezekana. Naamini wachezaji wetu wengi hawana uzoefu kama wapinzani wetu.

“Tulikuwa na lengo la kufika makundi tumetimiza na sasa tunataka kutetea ubingwa wa ligi ili tupate nafasi nyingine fa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema.

Kocha msaidizi

huyu hapa

Kwa sasa Patrick Aussems anasimama mwenyewe kwenye benchi la ufundi la Simba bila kocha msaidizi na hilo linaelezwa kuwa sababu ya matokeo mabovu.

Lakini, Mo ameeleza suala la kocha msaidizi ambaye ataungana na Aussems liko chini ya Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori. Tayari makocha watano wametajwa kuwepo kwenye orodha ya Simba. Makocha hao ni Denis Kitambi aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Sterwart Hall wakati huo wakiwa Azam na baadaye walienda wote FC Leopard ya Kenya ingawa kwa sasa hawapo nchini humo.

Wengine ni Salum Mayanga, ambaye ni Mkurugenzi wa benchi la Ufundi la Mtibwa Sugar, Seleman Matola anayeinoa Lipuli FC na Juma Mgunda wa Coastal Union.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa Kitambi ndiye anayepewa nafasi kubwa ukilinganisha na Mayanga, ambaye pia ni mkufunzi wa makocha.

Pia imeelezwa Matola na Mgunda pamoja na mapendekezo hayo bado kuna ugumu kupata nafasi labda ishindikane kumnasa Kitambi.

“Kwenye kikao chetu cha Bodi ya Wakurugenzi jukumu la kocha msaidizi anakabidhiwa Magori, tunaamini atapatikana kocha mzuri na atafanyiwa usaili kama ilivyokuwa kwa Aussems.

“Jukumu hilo linatakiwa kukamilika haraka iwezekanavyo tangu tulivyokubaliana,” alisema Mo Dewji, ambaye hakutaja wazi majina hayo ya makocha.