Mabeki washikilia ushindi Simba

Friday January 11 2019

 

By Charles Abel, Thobias Sebastian, Mwananchi

Dar es Salaam. Simba ina kila sababu ya kuibuka na ushindi katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura, lakini safu yake ya ulinzi inapaswa kuwa makini dakika zote 90 za mchezo huo.

Mabeki wa Simba wanapaswa kuwa makini na mshambuliaji nyota Mohamed Hammia ambaye ni tegemeo wa JS Saoura katika kufunga mabao na amekuwa chachu ya mafanikio katika kikosi hicho kwenye mashindano ya kimataifa.

Baada ya kuzing’oa Mbabane Swallows ya Swaziland na Nkana Red Devils kutoka Zambia, Simba imefuzu kucheza hatua ya awali ya mashindano hayo ambapo kesho itavaana na JS Saoura ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Rekodi maridadi ya Simba katika mashindano ya kimataifa pindi inapocheza nyumbani inaweza kuwa na mwendelezo mzuri mbele ya JS Saoura ambayo haifanyi vizuri ugenini.

Katika mechi tatu za mwisho za kimataifa ilizocheza Simba ikiwa nyumbani, imepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja huku ikifunga jumla ya mabao 10 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne.

Hata hivyo, Simba haipaswi kubweteka na rekodi kwa kuwa JS Saoura itakuja nchini ikitaka kufuta uteja wa kutofanya vyema katika mechi za ugenini.

JS Saoura haina rekodi nzuri ugenini kwasababu katika mechi tatu za kimataifa ilizocheza msimu huu na mwaka 2007, imetoka sare mara mbili, imefungwa mchezo mmoja, haina bao na nyavu zake zimetikiswa mara moja.

Kocha Patrick Aussems anatakiwa kuwa makini katika upangaji wa kikosi chake hasa kuimarisha safu ya ulinzi ambayo itakuwa chini ya Paschal Wawa na Juuko Murshid watakaocheza nafasi ya mabeki wa kati.

Beki kiraka Erasto Nyoni, ametibua hesabu za Aussems baada ya kuumia goti katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM, hivyo atamtumia Juuko kuziba pengo la mchezaji huyo. Nyoni atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tano.

Wawa na Juuko ambao uchezaji wao unafanana, wanatakiwa kuwa makini katika eneo la ulinzi kwa kucheza kwa nidhamu na tahadhari kubwa mbele ya Hammia.

Hammia ni mchezaji mjanja hana tofauti na Raheem Sterling wa Manchester City anapokuwa katikati ya mabeki wa timu pinzani au eneo la hatari.

Mshambuliaji huyo wa JS Saoura kama alivyo Sterling, ni mjanja wa kupitisha miguu kwa mabeki akiwa ndani ya eneo la hatari la timu pinzani ili kumshawishi mwamuzi kupata mkwaju wa penalti.

Pia Hammia ana tabia ya kujiangusha ndani ya eneo la hatari ili kumhadaa mwamuzi na katika kuthibitisha ujanja wake mabao manne iliyopata JS Saoura katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, matatu yalitokana na penalti baada ya kujiangusha.

Safu ya ulinzi ya Simba inapaswa kuwa makini zaidi na mbinu ya kupiga mashuti ya mbali inayotumia JS Saoura hasa katika mechi ambazo inakuwa imezidiwa.

JS Saoura imekuwa ikimtumia kiungo mshambuliaji Messalla Merbah mwenye umri wa miaka 27 ambaye ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali nje ya eneo la hatari anapopata nafasi ya kupenya ngome ya wapinzani.

Pia Simba inapaswa kuwa makini na mawinga Younes Koulkheir na Hamza Zaidi ambao wana uwezo wa kuingia ndani kucheza kama viungo wanapokutana na timu imara sehemu ya katikati.

Wachezaji wa JS Saoura ni hodari katika kufunga mabao kupitia mipira ya kona na adhabu ndogo kwenda langoni mwa wapinzani, hivyo Simba inapaswa kuwa makini muda wote.

Kwa upande wa Simba imekuwa ikibebwa na mbinu mpya ya kushambulia kwa kushitukiza wakiingia kwa haraka eneo la timu pinzani, baada ya kupoka mpira na wakati mwingine hutumia mbinu ya kupiga pasi nyingi fupi ili kujenga mashambulizi.

Timu hiyo inatarajiwa kutumia mfumo wa 4-3-3 kwa kuendelea kuwapanga Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco upande wa ushambuliaji, nyuma yao wakiwepo, Jonas Mkude James Kotei na Chama katika eneo la kiungo.

Mfumo huo umekuwa ukibadilika hasa pale wanapoingia Shiza Kichuya anayetokea pembeni na Hassani Dilunga ambapo hucheza mfumo wa 4-4-2.

Wadau walonga

Kocha Joseph Kanakamfumu alisema ana amini uzoefu wa Wawa na Juuko utakuwa dawa ya kuwadhibiti washambuliaji wa JS Saoura.

“Sioni tatizo sana kwa mabeki wa Simba kuwadhibiti Saoura hasa huyo mshambuliaji wao kwa sababu Juuko ni mnyumbulifu na washambuliaji wa kiafrika siyo kama wale wa Ulaya ambao wanamfuata beki mguuni pindi wanapokuwa na mpira.

“Naamini kama Juuko akirekebishwa kidogo sioni ni wapi hao washambuliaji wa timu pinzani watapitia,” alisema Kanakamfumu ambaye pia ni mchambuzi wa soka.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema mbinu bora ya kuwadhibiti washambuliaji wa timu za kiarabu ni umakini na nidhamu.

“Wanapaswa kucheza kwa nidhamu na umakini wa hali ya juu dakika zote za mchezo na wasifanye makosa ambayo yanaweza kuwapa nafasi wapinzani wao. Waarabu ni wajanja wanafahamu vyema kutumia makosa ya timu pinzani,” alisema Pawasa.

Thamani

Simba ina shauku ya kuwazima nyota wa JS Saoura ambayo thamani yake ni Euro 7.2 milioni (zaidi ya Sh18 bilioni za Tanzania).

Kikosi cha kwanza JS Saoura kinachoundwa na kundi kubwa la nyota kutoka Algeria kina thamani ya Sh9.1 bilioni, fedha ambayo ni mara nane ya thamani ya Simba Sh1.3 bilioni.

Mchezaji ghali Simba ni Chama ambaye mtandao wa ‘Transfermarkt’ umemtaja ana thamani ya Euro 100,000, lakini JS Saoura ni Merbah ana thamani ya Euro 500,000 (zaidi ya Sh1.3 bilioni).

Mchezaji mwenye thamani ya chini katika kikosi cha Simba ni Nyoni Sh35 milioni, JS Saoura ni beki Nacereddine Khoualed Euro 200,000 (zaidi ya Sh524 milioni).

Advertisement