Macho yote kwa Serengeti Boys

Sunday April 14 2019

 

By Charles Abel, Mwananchi

Dar es Salaam. Hatimaye kipenga cha kuashiria kuanza kwa fainali za Afrika kwa vijana wa U-17 (Afcon) kitapulizwa leo kuanzia saa 10:00 kati ya Tanzania na Nigeria.

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ambaye ndiye mgeni rasmi, ataongoza mashabiki wa soka katika kuipa nguvu Serengeti Boys.

Fainali hizo zinashirikisha timu nane ambazo ni wenyeji Tanzania, Nigeria, Uganda, Angola, Senegal, Guinea ,Morocco na Cameroon.

Serengeti Boys iko tayari kwa mashindano hayo na kocha mkuu wa kikosi hicho Oscar Mirambo ametamba kuwa vijana wako vizuri tayari kuweka historia mpya ya kufuzu Kombe la Dunia.

Mipango ya kiufundi ya benchi la ufundi la Serengeti Boys chini ya Mirambo ni wazi kwamba vinaiweka Serengeti Boys kwenye nafasi nzuri kisaikolojia kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Licha ya wengi kuitazama Nigeria kama moja ya timu tishio kwenye mashindano hayo, kocha Mirambo ameshtukia kuwa nguvu ya timu hiyo ipo kwa wachezaji wawili ambao kama watadhibitiwa vilivyo basi shughuli ya kuwamaliza vijana hao wa Nigeria itakuwa nyepesi.

“Nimepata nafasi ya kuwafuatilia na kuwafanyia tathmini Nigeria. Nilichogundua wamekuwa wakipendelea mfumo wa 4-3-3 na kuna mshambuliaji wao mmoja mwenye kasi ambaye ndiye wamekuwa wakimtumia kusaka mabao yao kwa kumpigia mipira mirefu ambayo amekuwa akiitumia kufunga na kuzalisha mabao kutokana na kasi yake pamoja na kiungo wao mahiri.

“Tumeshalifanyia kazi hilo na tumejipanga kwanza kuhakikisha huyo kiungo hapati mwanya wa kumchezesha huyo mshambuliaji wao lakini pia kumzima yeye mwenyewe kwani ukikamata hao, umeua nguvu yote ya Nigeria,” alisema Mirambo. Kwa upande wake nahodha wa Serengeti Boys, Abraham Morice alisema timu iko tayari kwa ajili ya mashindano

hayo. “Tumepata maandalizi mazuri na tuko tayari kuwakabili Nigeria. Sisi kama wachezaji hatuwahofii na tunejipanga vyema kupata ushindi dhidi yao.

Tunaamini utejeo wa mwenzetu Kelvin John umetupa hamasa na molali zaidi ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya,” alisema Abraham.

Hata hivyo, maandalizi yao yamenogeshwa zaidi na ahadi ya kila mchezaji kupewa gari na Sh20mil kwa Mwenyekiti na Mtendaji wa Kampuni za IPP, Mzee Reginald Mengi iwapo watamaliza nafasi mbili za juu.

Wakati huo huo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amekabidhi hundi ya Sh10 milioni kwa Yabaridi Band ya Dar es Salaam kwa kushinda wimbo wa kuhamasisha Serengeti Boys kwenye Afcon ya mwaka huu.

Advertisement