Madam Ritha kuhusu kuachana na shindano la BSS

Tuesday September 17 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa shindano la Bongo Star Search(BSS) nchini Tanzania, Rita Paulsen amesema katika kipindi cha miaka 10  ya kufanyika kwa shindano hilo wamepigwa vita hadi kufikiria kuachana nalo.

Rita kwa jina maarufu la Madam Ritha ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 17, 2019 alipokuwa akitangaza kuanzia kwa  msimu wa kumi wa shindano hilo.

Madam Ritha amesema pamoja na kuwepo na mawazo ya kuacha walijikuta wakiendelea kwa kuwa kazi hiyo kwao ni wito.

"Sisi ndio tunaojua namna gani BSS imebadili maisha ya watu hivyo tuliona tukiacha kuendelea na shindano hili wapo watakaoathirika licha ya vita tuliyopigwa ikiwemo kuambiwa hakuna staa wa maana tuliyemtoa.”

"Lakini ukweli ni kwamba hadi sasa tumebadili maisha ya watu zaidi ya 200 na tumeweza kuaminiwa na kufanya kazi na kampuni zaidi ya 50,000 hivyo maneno ya watu hayaturudishi nyuma zaidi ya kutufanya tusonge mbele, " amesema Ritha.

Kwa upande wake, Haji Ramadhani ambaye ni mshindi wa BSS 2011 akitoa ushuhuda namna shindano hilo limemnufaisha amesema mbali na kupata ajira katika bendi ya Twanga pia lilimuwezesha kwa mara ya kwanza kupanda ndege kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam.

Advertisement

Haji amesema alipoingia katika shindano hilo malengo yake hayakuwa kushindwa Sh50,000 bali  kuonekana na anashukuru leo maisha yake yamebadilika na anaweza kwenda kokote akasikilizwa.

Advertisement