Magori afungukia Bocco kusaini Polokwane City

Tuesday June 11 2019

 

By THOMAS NG'ITU

Dar es Salaam. Utata utatani unaambiwa, mshambuliaji John Bocco ameiingiza katika vita klabu yake ya Simba na ile Polokwane City inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini baada ya kusaini mikataba na klabu hizo.

Iko hivi baada ya Simba jana kuachia picha zikimuonyesha mshambuliaji huyo akisaini mkataba mpya ndio habari za nahodha huyo kusaini mkataba na Polokwane zikaibuka.

Mtendaji mkuu wa Simba, Crescentius Magori alikaliliwa akizungumza na kituo cha Redio EFM, alisema ni kweli Bocco alisaini mkataba wa awali, lakini hakufuata taratibu.

Magori alisema anajua kabisa kwamba mchezaji huyo alisaini mkataba wa awali, lakini hilo halikuwazuia wao kumpa mkataba mpya kwasababu bado alikuwa katika mkataba wao.

"Polokwane walikosea kwa sababu hawakufuata taratibu, walijua tayari tumeshamsaini, lakini wao naona walikuwa wanataka kama ushindani na sisi, hata huyo wakala sisi tulimuambia kabisa kwamba tayari tumemalizana," alisema Magori.

Aliongeza kwamba kuhusu suala la mkataba wa awali hata wao walimsainisha mshambuliaji wa Ndanda, Vitalis Mayanga, lakini siyo mchezaji wao.

Advertisement

"Mkataba wa awali unakua unamuonyesha mchezaji uhakika wa yeye kuhitajika, hao Polokwane wamempa Bocco mkataba juu ya mkataba kitu ambacho wamekosea na kama PSL wamepokea mkataba basi Fifa itahusika," alisema.

Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu kwamba Bocco alisaini mkataba wa awali na Polokwane usiku mara baada ya kumalizika pambano la Simba na Mazembe, huku mkataba wa Simba akisaini Mei 17.

Mkataba wa awali alioingia Bocco na Polokwane unaonyesha unaanza rasmi Julai 1, 2019 na kumalizika Juni 31, 2021.

Advertisement