Magufuli: Tusiwabeze Taifa Stars tuwape moyo

Muktasari:

  • Taifa Stars ilianza vibaya katika fainali hizo baada ya kufungwa mabaoi 2-0 na Senegal kumeibua mijadala mingi kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka nchini.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amewatia moyo wachezaji wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ akiwataka waendelee kupambana licha ya kuanza vibaya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Akizungumza katika ufunguzi wa kampuni ya gesi Taifa gesi, Kigamboni, Dar es Salaam leo baada ya kuombwa atoe neno na mkuu wa mkoa Paul Makonda kuhusu timu ya Taifa Rais Magufuli alisema vijana waendelee kupambana.

"Mwanzo siyo mbaya kwa kufungwa na timu inayoongoza Afrika tena kwa kufungwa 2-0 na Senegal ambayo wachezaji wao wote wakiwa wanacheza Ulaya," alisema.

Alisema huu ni muda wa wachezaji kupewa moyo wa kuendelea kufanya vizuri katika fainali hizo zinazoendelea nchini Misri.

"Wachezaji wapewe moyo kwa sababu wakifungwa tunafungwa Tanzania na wakishinda basi inashinda Tanzania, kwenye uwanja wa mpira kuna kushinda na kushindwa sisi tutaendelea kuwaombea," alisema Rais Magufuli.

Rais alimruhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuondoka na kwenda Misri kwa ajili ya kuongeza motisha kwa wachezaji.

Taifa Stars kwa sasa inajiandaa na mchezo wa pili dhidi ya Kenya utakaochezwa Alhamisi ikiwa na lengo la kushinda ili kurudisha matumaini yake ya kusonga mbele.