Maguire ageuka lulu Man United

Muktasari:

  • Beki mpya wa Manchester United, Harry Maguire amegeuka lulu baada ya kucheza kwa kiwango bora katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea.

London, England. Harry Maguire amethibitisha ubora wake baada ya  kucheza vyema mechi yake ya kwanza dhidi ya Chelsea jana usiku.

Jose Mourinho amemtaja Maguire ndiye mchezaji bora wa mechi hiyo ambayo Manchester United ilishinda mabao 4-0.

Maguire ametua Old Trafford katika usajili wa majira ya kiangazi akiwa ndiye beki ghali duniani akinunuliwa kwa Pauni80 milioni akitokea Leicester City.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa England amempiku Virgil van Dijk wa Liverpool aliyekuwa beki ghali alipotua ndani ya klabu hiyo misimi miwili iliyopita akitokea Southampton kwa Pauni75 milioni.

Maguire aliituliza ngome ya Man United licha ya kucheza mechi yake ya kwanza tena yenye ushindani mkali.

Kocha huyo wa zamani wa Man United na Chelsea, alisema beki huyo wa kati alicheza kwa kiwango bora.

“Nadhani anastahili kuwa mchezaji bora wa mechi. Alicheza kwa ubora na kiongozi ndani ya timu, aliipa timu kujiamini,” alisema Mourinho.

Alisema ngome inapokuwa imara timu inakuwa na nafasi ya kupata matokeo mazuri kwa kuwa haichezi kwa presha tofauti na mabeki wanapokuwa wanafanya makosa mara kwa mara.

Maguire amekwenda kujaza nafasi ya Eric Bailly ambaye atakuwa nje ya uwanja miezi minne baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.