Maisha ya Samata mkubwa Bongo

WAHENGA wanasema nyota njema huonekana asubuhi ndivyo yalivyokuwa maisha ya Mohamed na Mbwana vijana wa mzee Ali Pazi Samatta, walicheza soka la kitaa pamoja na timu ya Ligi Kuu Bara ambayo ni African Lyon.

Mohamed (31), ni mchezaji wa KMC na ni kaka yake na Mbwana ambaye ni straika wa Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL), na wote wakiwa wadogo nyota zao zilikuwa tofauti.

Wanaitana swahiba kutokana na kukua pamoja na kuchezea baadhi ya timu za mitaani pamoja, lakini Mbwana alionekana nyota yake kuwa na kibali cha kufika mbali kuliko kaka yake, Mohamed.

Mwanaspoti lilimtembelea Mohamed nyumbani kwao Mbagala Rangi Tatu na kufanya naye mahojiano ambapo linakuletea vitu ambavyo hujawahi kusikia kutoka kwake.

MIAKA 11 BARA, DAU MILIONI 28.8

Tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara huu ni mwaka wa 11 kwa Mohamed, na alianzia Lyon ambako alisaini mkataba wa miaka mitatu kwa dau la Sh800,000 (laki nane) na mshahara akawa anapokea Sh200,000.

Jumla ya dau lake tangu aanze kucheza ligi 2007/20 ni Sh28.8 milioni. Baada ya Lyon kushuka alikwenda kujiunga na Mgambo JKT ambayo aliichezea msimu wa 2013/16 ambako dau lake lilikuwa Sh4 milioni na alianza na mshahara wa Sh250,000 ukapanda mpaka Sh300,000.

Ni Kama alikuwa na gundu kwani Mgambo JKT nayo ilishuka ndipo akatimkia Tanzania Prisons ambako alicheza msimu wa 2016/17 dau lake lilikuwa Sh11 milioni na mshahara alianza na Sh500,000 ukapanda mpaka 700,000.

Baadaye Mbeya City ikamfuata na dau nono zaidi la Sh9 milioni na mshahara wa Sh1 milioni akasaini miaka miwili katika msimu wa 2017/19, akacheza miezi sita mwingine kwa kulipwa mshahara hapo hapakuwa na dau.

“Msimu huu nimesaini mkataba wa miaka miwili KMC kwa dau la Sh8 milioni na mshahara wangu ni Sh700,000,” anasema.

“Sidhani kama kuna mchezaji ambaye amewahi kuweka mshahara wake wazi, nafanya hivi ili kuwafunza wengine wanaokuja nyuma yangu ili watie bidii nakuamini ipo siku nitafanikiwa.”

Anasema licha ya kuzaliwa tumbo moja na Mbwana, anaamini Mungu anajua kugawa mafungu ya riziki na kusisitiza kuwa hataki kutembelea nyota ya mdogo wake.

“Ingawa kuna wakati watu wakisikia Mudi Samatta wananiuliza umezaliwa naye, wanaona siendani naye sijui, najibu ndio mama mmoja baba mmoja,” anasema.

LAKI 8 TU ALIJAZA GHETO

Baada ya Mbagala Market kupanda Ligi Kuu na kuitwa African Lyon, ikiwa imenunuliwa na Mohammed Dewji ‘MO’, Mohamed alisaini mkataba wa miaka mitatu kwa kiasi cha Sh800,000.

Hiyo ilikuwa pesa yake kubwa kuishika kwa wakati huo, anasema hakutaka kujiuliza mara mbilimbili baada ya kuambiwa akasaini na mshahara alikuwa analipa Sh200,000.

“Baba nilimpa Sh50,000, nikanunua viti vya makochi vya laki mbili na themanini, mito nilinunua laki moja na nusu, simu ya elfu sitini na kapeti la elfu thelathini,” anasema

“Gheto langu likapendeza na ilinipa moyo kupenda soka na kuamini litakuwa linainua kipato cha uchumi wangu.”.

SAMAGOL AMZIDI UJANJA

Anasema walisaini na mdogo wake Mbwana mkataba wa miaka mitatu pale Mbagala Marjet ila malipo yalikuwa tofauti, ambapo ndugu yake dau lilikuwa Sh3 milioni na mshahara Sh300,000.

“Tangu tukiwa wadogo Mbwana si mtu wa kuyumbishwa, African Lyon wakati timu inapanda yeye alikuwa ndiye staa, hiyo milioni tatu alikuwa anagoma, mshahara wake ukawa Sh300,000 hapo tulijisimamia wenyewe hapakuwa na meneja wala baba yetu, ambaye kawaida yake anatuambia kapambane nawaaminia,” anasema.

“Bahati nzuri akaondoka na kwenda Simba, kisha TP Mazembe, Genk na sasa Aston Villa, hivyo nyota yake iling’ara kuliko mimi toka zamani tofauti na wanavyomdhania.”

UBORA WA SAMAGOL KWAKE

Mohamed anasema laiti kama wadau wa soka wangemuona Samatta yule ambaye alikuwa anacheza mchangani wakiwa wadogo, basi huyu wangemuona ‘chamtoto.’

Anasema kwamba kwa sasa soka analocheza Mbwana linachanganywa na sayansi na teknolojia, hivyo anakosa uhuru kama alivyokuwa kitaa.

“Samatta bora kwangu, ni yule niliyekuwa nacheza naye mchangani, alikuwa anaupiga mwingi kwani hakuwekewa mipaka pa kuishia tofauti na sasa ambapo lazima afuate kile anachoambiwa na kocha wake,” anasema.

AMEZIDIWA KIPAJI

Mohamed anasema anasikia maneno ya watu wanaosema yeye ana kipaji kuliko mdogo wake, jambo ambalo amelipinga na kusisitiza kwamba ni bora wazungumze wale waliokuwa wanawaona wakiwa wadogo.

“Mfano mtu wa kwanza kumwambia mzee kwamba Mbwana atafika mbali ni kocha Maka Mwalusi ambaye amewafundisha kaka zangu, hakusema mimi, hilo linadhihirisha aliona kitu kwenye mguu wake.”

MECHI WALIZOCHEZA PAMOJA

Mohamed anasema wakati wakiwa African Lyon mechi ya kwanza kucheza na mdogo wake ni dhidi ya Yanga na matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ilikuwaje?Anaeleza kwamba mdogo wake alicheza namba tisa, yeye namba nane na walifurahia kuona ndoto yao inakwenda kuwa kubwa.

“Ulikuwa msimu wa 2009/12, sitakaa niisahau siku hiyo, nilicheza dakika 80 Mbwana alicheza 90 kwa kiwango cha juu,” anasema Mohamed.

“Katika msimu huohuo Mbwana alimaliza na mabao manane pasi nne za mabao nilitoa mimi, bahati nzuri akaonekana na Simba ikamsajili.”

MAISHA YA UTOTONI

Anasimulia kwamba utotoni yalikuwepo maisha ya furaha na huzuni na kwamba ilikuwa ngumu kuwatofautisha kwa kuwa muda mwingi walikuwa pamoja. “Siwezi kusema nilikuwa namchapa, yeye ana mwili mkubwa tangu zamani, hivyo kuna wakati tulikuwa tunapigana,,wakati mwingine tunacheka, ujue haniiti kaka ananiita swahiba,” anasema.

KILICHOMSHANGAZA

Mwaka 2000 mama yao mzazi alifariki dunia na Mohamed alikuwa darasa la saba huku Mbwana akiwa la tatu. “Mama alikuwa anaumwaumwa, siku hiyo nikawa nimetoka shule, nikagonga chumbani kwake nikakuta kumefungwa, moyo ukawa na wasiwasi kwamba hali si shwari, baadaye baba akaja chumbani kwangu akakuta najisomea akamuuliza kaka yangu mkubwa Sad yupo wapi nikamjibu sijui,” anasema Mohamed.

“Alivyotoka nikaenda uwanjani nilipokuwa nacheza mechi, baadaye akaja Mbwana, nikawa namsimulia kwamba hali ya mama si nzuri, akanijibu amefariki akaendelea kucheza na wenzake, nikawa najiuliza mbona katamka neno zito halafu hana wasiwasi.”

Anaongeza kuwa: ”Nikaamua kurejea nyumbani nikakutana na gari limebeba mwili wa mama, ndipo nikagundua alichosema Mbwana cha kweli.”

Mwanasoka huyo anasema kuna wakati akikumbuka tukio hilo anabaki kushangaa na anaamini hata akimuuliza mdogo wake hana hakika kama atakumbuka.

ADHABU YA PENALTI

Mohamed anasema wakati wakiwa wadogo baba yao alikuwa anawaonyesha wachezaji wanaokosa penalti kwamba ni kipi walitakiwa wakifanye ili wao wafunge na wakikosa wanatozwa ‘faini’.

“Ni kitu ambacho ametufundisha sana, tulianza kulipa (pesa) tukiwa tunacheza huko mchangani, ilikuwa Sh2,000 baadaye Ligi Kuu ikawa 5,000 na sasa tunalipa 10,000 na mimi nadaiwa,” anasema.

“Tulikuwa na tabia ya kusemeleana tukiwa wadogo, mfano Mbwana akikosa penalti namwambia baba (Mbwana) kakosa penalti na hapo (baba) ana pesa, basi anamwambia nipe changu.”

Anapoulizwa juu ya Mbwana ni mtu wa aina gani, Mohamed anasema ni kijana mwenye aibu iliyopitiliza na hapendi uchafu, kubwa zaidi anapenda kwenda na muda.

“Tangu (tukiwa) wadogo baba alitufundisha kwenda na muda, hilo limeongezeka kwa mdogo wangu na hataki mambo ya kupindapinda,” anasema.

“Akikuambia nitafanya jambo fulani analifanya, naona anazidi kuzingatia vitu kuliko mwanzo.”

WANAPOKUTANA

Anasema wanapokutana na mdogo wake anapoulizwa anamwambia nini kuhusu kazi zake? Anaanza kwa kicheko kisha anasema, “ananisisitiza kuamini katika kile ninachokifanya. Nagundua anafuatilia kazi zangu, huwa nikifunga (bao) nakuta amenitumia video kisha ananiambia hongera kwa kazi nzuri, alivyo Mbwana hafanyi wanachopenda watu anapenda kutimiza majukumu yake.”

KUNYANYAPALIWA

Wakati anasimulia changamoto anazokutana nazo uwanjani ghafla sura yake ikaonyesha unyonge kwa namna anavyoumizwa na maneno ya baadhi ya wachezaji. “Huwa nakutana na maneno ya karaha, wapo wanaosema ‘ndugu yako bahati tu hana lolote’, wapo wanaoninyanyapaa na kuonyesha kwamba sina lolote, siwezi kufikia kiwango chake wala anga zake alipo sasa na nyota yake inang’ara yangu imefifia. Hayo maneno yanagusa moyo wangu nakuwa sina cha kufanya, huwa nakaa kimya,” anasema.

“Siwezi kutamani kuwa kama Mbwana, natamani kuwa mimi kwani yule ni mdogo kwangu, hivyo siwezi kusema nataka kufika alipo yeye, napambana kwa kadri ninavyoweza.”

MJENGO WAKE

Mohamed ambaye anaishi kwenye mjengo wake uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, anasema haikuwa rahisi kujenga, lakini kutokata tamaa ndiko kumefanikisha jambo hilo.

“Msimu wa kwanza Mbwana kucheza Simba nilimwambia kuna uwanja unauzwa Sh2 milioni akanisaidia Sh800,000, nyingine nikajitafutia mwenyewe mpaka nikamaliza, maana nilikuwa nalipa kidogo kidogo,” anasema. “Katika harakati zangu za kusajiliwa huku na kule nikawa najenga mpaka nimehamia, hata nikija kupata pesa kubwa sitakaa nihame kwani nimeitolea sana jasho (nyumba hii).”

NDINGA ANAYOMILIKI

Mohamed anasema anatumia gari aina ya Vitz aliyonunuliwa na mdogo wake Mbwana. “Hiyo ndio gari yangu ya kwanza, siwezi kusema sio mpenzi wa magari wakati sina pesa, ngoja nizishike nitaijua tabia yangu, kuhusu simu natumia Tecno.”

MAPENZI YALIMUUMIZA

Kabla ya kuoa, mke wake Nuru Ramadhani alikuwa na mchumba wake aliyekaa naye miaka mitatu na wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume anayeitwa Razack (8), lakini ghafla penzi lao likaingia ‘mchanga’.

Anasema hawezi kumhukumu moja kwa moja mzazi mwenzake kwa kuwa inawezekana umbali ndio ulikuwa chanzo cha kutafuta mwanaume mwingine.

“Kipindi hicho nilikuwa JKT Mgambo, nilikuwa naambiwa ‘na mchumba wako ana mtu’ mara vile kama haitoshi akaja akanithibitishia mwenyewe baadaye kila kitu, iliniumiza na kunipa maswali mengi kwamba kwa nini kafanya hivi,” anasema.

FAMILIA, MKEWE ANENA

Mohamed ana mke aitwaye Nuru na watoto wawili, Razack (8) na Rihama (3).

Mkewe Nuru anasema alikumbana na wakati mgumu wakati shemeji yake Mbwana anaoa ambapo ilikuwa harusi ya kimyakimya, lakini baadhi ya watu wakaunganisha matukio na kuweka picha yake wakidai ndiye mke wa supastaa huyo anayecheza Aston Villa.

“Sikuwa na furaha kwa sababu nilikuwa nashangaa watu wana shida gani, baadaye shemeji Mbwana akaniambia niachane na mambo ya mitandao niangalie mume wangu anafanya nini kwangu,” anasema Nuru.

Mbali na hilo, anasema anatamani kumuona mumewe anafika mbali kisoka. “Ingawa mume wangu hapendi niende uwanjani kumsapoti nakuwa namuombea Mungu amfungulie milango, naamini ipo siku atafanya maajabu.”