Makambo, Kagere watwishwa zigo

Dar es Salaam.Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya kuchezwa mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba, kivutio katika mchezo huo kitakuwa kwa washambuliaji Heritier Makambo na Meddie Kagere.

Makambo na Kagere wamekuwa chachu ya mafanikio ya timu zao katika mashindano yote msimu huu kutokana na uwezo wao wa kufunga mabao.

Makambo raia wa DR Congo, ndiye shujaa wa Yanga akiongoza kwa kufunga mabao 11 na Kagere anashika nafasi ya sita kwa mabao manane katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Makambo amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga ingawa katika mechi tatu za mwisho hakuwa katika kiwango bora kiasi ambacho kilimshitua kocha Mwinyi Zahera.

Hata hivyo, Makambo anaweza kuibuka shujaa katika mechi ya kesho na kuwanyamazisha mashabiki wa Simba wanaombeza, lakini atakuwa na kazi ngumu kuwapita mabeki watukutu Pascal Wawa na Juuko Murshid.

Kagere atakuwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki wababe Kelvin Yondani na Andrew Vincent na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Bao pekee alilofunga dhidi ya Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huenda ikawa imeongeza morali kwa Kagere kuilaza mapema Yanga katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.