Makambo chini ya ulinzi wa Wawa, Juuko

Muktasari:

Kitendo cha Heritier Makambo kusimama peke yake katika eneo la ushambuliaji, kumewafanya mabeki wa Simba wasiwe na kazi ngumu ya kuzuia mashambulizi.

Dar es Salaam. Kitendo cha kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kumchezesha Heritier Makambo kama mshambuliaji pekee kuliwafanya mabeki wa Simba wasiwe na kazi kubwa ya kufanya.

Mabeki wa Simba wakiongozwa Pascal Wawa na Juuko Murshid walikuwa makini kumdhibiti Makambo ambaye hakuonekana kabisa kufurukuta ndani ya dakika 45.

Licha ya Amis Tambwe kuwepo katika eneo la ushambuliaji, hakuweza kusimama zaidi katika eneo la ushambuliaji badala yake alikuwa akitokea katikati na kusogea juu kitu ambacho kiliwapa nguvu Simba kuzuia bila wasiwasi.

Hata hivyo Yanga waliamua kutumia mipira ya pembeni kupitia kwa Paul Godfrey kupeleka mashambulizi, lakini bado krosi ambazo zilikuwa zinapigwa hazikuweza kuzaa bao lolote.

Simba wao katika eneo la ushambuliaji walianzisha washambuliaji wawili na walionekana zaidi kushambulia mfululizo katika goli la Yanga, hata hivyo hawakuweza kupata bao ndani ya dakika 45.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo ni 0-0.