Makocha Ligi Kuu kitanzini

Dar es Salaam. Wakati ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulioanza mapema ukigeuka kivutio, hali hiyo inayaweka maisha ya makocha kitanzini msimu huu.

Idadi kubwa ya makocha wanalazimika kufanya kazi ya ziada kuzipa matokeo mazuri timu zao vinginevyo wanaweza kujiweka katika hatari ya kutimuliwa.

Panga la mapema ambalo limekata vichwa sita vya makocha katika Ligi Kuu, linatoa ishara ya wazi msimu huu unaweza kuwa mgumu kwa maisha ya makocha.

Kabla msimu wa ligi haujafikisha theluthi moja ya mechi zote, makocha sita tofauti wameshatimuliwa na klabu zao huku baadhi waliobaki wakiwa wamekalia kuti kavu.

Nuksi kwa makocha ilianza kwa Athumani Bilali aliyetimuliwa mapema zaidi na Alliance FC baada ya kuiongoza katika mchezo mmoja tu wa ligi ambao ulikuwa dhidi ya Mbao waliotoka sare ya bao 1-1.

Upepo mbaya ulihamia kwa Fred Felix ‘Minziro’ ambaye baada ya timu ya Singida United aliyokuwa akiifundisha kupoteza mechi mbili dhidi ya Mwadui na Namungo uongozi ulimuondoa na kumleta Ramadhani Nsanzurwimo kutoka Burundi anayeinoa hadi sasa.

Kocha wa tatu ni Amri Said ‘Stam’ alitimuliwa Biashara United ya Mara kutokana na mwenendo usioridhisha katika mechi nne za kwanza za timu hiyo dhidi ya Kagera Sugar, Mbao, Alliance na JKT Tanzania ambapo ilipoteza tatu zote ikicheza uwanja wa nyumbani na kupata sare moja tu.

Vita ya kuwania ubingwa, kanuni ya timu za mwisho katika msimamo wa ligi kushuka daraja moja kwa moja, mbili za juu ya hizo kucheza mechi za mchujo na maandalizi ambayo kila timu ilifanya kabla ya msimu kuanza, ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuwaweka makocha katika presha kubwa.

Mkosi huo ulihamia kwa kocha Malale Hamsini wa Ndanda ambaye kipigo cha bao 1-0 kutoka Mtibwa Sugar katika raundi ya sita kilimponza.

Kabla ya mchezo huo aliiongoza Ndanda katika mechi tano ambazo ilitoka sare mara tatu na kupoteza mbili.

Bundi huyo alitulia kwa muda kabla ya kuibuka mwezi huu kwa makocha Mwinyi Zahera wa Yanga na Jackson Mayanja wa KMC.

Novemba 5, Yanga iliachana na Zahera kwa kile ilichodai kutoridhishwa na kiwango cha timu hasa baada ya kutolewa katika hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 5-1.

Siku tano baada ya Zahera kutimuliwa, Mayanja alitupiwa virago KMC, kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika ligi.

Hadi KMC inaachana na Mayanja ilikuwa imeibuka na ushindi katika mechi mbili tu za ligi, ikitoka sare mbili na kupoteza nne.

Wakati makocha hao sita wakiwa wamefungashiwa virago mapema, wengine wapo katika presha kutokana na mwenendo wa timu zao katika ligi kutovutia.

Makocha hao ni Nsanzurwimo wa Singida United, Juma Mwambusi (Mbeya City), Khalid Adam (Mwadui) na Juma Mgunda wa Coastal Union kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu zao katika ligi.

Akitoa maoni yake, Bilali alisema viongozi wa klabu wamekuwa chanzo cha makocha kuondolewa bila sababu za msingi.

“Wakati mwingine makocha hatuna matatizo, viongozi ndio chanzo. Wamekuwa wakiingilia majukumu ya benchi la ufundi na timu inaposhindwa kufanya vizuri badala ya kuwajibika wanahukumu makocha,” alisema Bilali.

Mchambuzi Alex Kashasha alisema utamaduni wa kutowapa makocha muda wa kufanya kazi utaendelea kulitafuna soka la Tanzania.

“Tumekuwa tukijiaminisha makocha kuwa wanaajiriwa ili watimuliwe dhana ambayo imekuwa ikitumiwa na klabu zetu lakini ukiangalia utabaini makocha hawapewi nafasi ya kutengeneza timu jambo ambalo linahitaji muda. Kwa hali kama hiyo tutaendelea kutimua walimu kila kukicha pasipo kutibu tatizo,” alisema Kashasha.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Idd Kipingu alisema mfumo wa soka unawapa wakati mgumu makocha kutekeleza majukumu kwa muda wanaopewa.

Alisema idadi kubwa ya makocha wanaotimuliwa nchini wanaingia mikataba isiyokuwa na tija. “Baadhi ya makocha waningia mikataba ya muda mfupi ambayo hawapi nafasi ya kujenga timu imara”, alisema Kipingu.