Makonda aanika mikakati mitano ya kuimaliza Uganda

Muktasari:

  • Ushindi wa Stars dhidi ya Uganda utaivusha kwenda fainali za AFCON mwaka 2019, pia itapaswa kuombea Cape Verde iibuke na ushindi au kutoka sare na Lesotho.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Paul Makonda ametaja mikakati mitano ya kuhakikisha timu hiyo inaibuka na ushindi dhidi ya Uganda, Jumapili Machi 24.

Stars inalazimika kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo na kisha kuombea Lesotho ifungwe au kutoka sare na Cape Verde ili iweze kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Juni nchini Misri.

Akizungumza leo, Makonda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema ikiwa mikakati hiyo mitano itafanyiwa kazi, safari ya kwenda AFCON itakuwa nyepesi.

"Kwanza ningependa kuona tukihudhuria kwa wingi pale Uwanja wa Taifa kwa sababu uwingi wetu utaongeza molali, lakini pili ni kuomba tukiingia pale tuwe wachezaji wa 12.

“Pia, tunapaswa kuwa kitu kimoja na kuweka kando utofauti wa kitimu na kingine ni waandishi wa habari kutoa nafasi kwa habari zinazohusu timu ya Taifa na jambo la tano ni viongozi wa dini, wasanii na viongozi wa kisiasa kuhamasisha kwa nafasi yao," alisema Makonda.