Man City yawatega Sterling, Aguero

Muktasari:

  • Mtendaji Mkuu wa Manchester City Ferran Soriano amesema ana matumaini wachezaji nyota wa timu hiyo watabaki ndani ya klabu hiyo licha ya kufungiwa na Uefa.

London, England. Manchester City ina matumaini Pep Guardiola na wachezaji nyota watabaki ndani ya klabu hiyo licha ya kufungiwa miaka miwili kushiriki mashindano ya Ulaya.

Raheem Sterling amekuwa mchezaji wa kwanza kutamka kuwa atabaki Man City licha ya kutakiwa na Real Madrid.

Shirikisho la Sola Ulaya (Uefa) limeifungia Man City miaka miwili kushiriki mashindano ya Ulaya kutokana na kukiuka sheria ya matumizi ya usajili mwaka 2012 na 2016.

Hata hivyo, Man City imepewa nafasi ya kukata rufani kupinga adhabu hiyo  ambayo imeibua hofu ndani ya klabu hiyo ya Etihad.

Juzi Jumamosi Guardiola aliwaambia wachezaji wake kujikita katika maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid itakayochezwa keshokutwa Jumatano.

Mtendaji Mkuu wa Man City Ferran Soriano ana imani mastaa wa timu hiyo watabaki Etihad wakati suala lao liko mikononi mwa Uefa.

Sterling, Kevin De Bruyne na Bernardo Silva ni miongoni mwa nyota wanaowindwa na klabu za Ulaya katika usajili wa majira ya kiangazi.

Pia wachezaji watatu Sergio Aguero, Fernandinho na Leroy Sane watakuwa nje ya mkataba mwishoni mwa msimu ujao. Wakati Uefa imeshusha rungu Man City, Guardiola amewekewa donge nono na ‘Kibibi Kizee’ cha Turin Juventus.