Mane: Uchovu upo ila Chelsea sitaki kuwakosa

Muktasari:

Mane aliisaidia Liverpool msimu uliopita kumaliza nafasi ya Ligi Kuu England huku wakitwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuifunga Tottenhma katika fainali iliyofanyika jijini Madrid.

London, England. Mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane anadai kuchoka kiakili lakini yupo tayari kuanza leo katika mchezo wa UEFA 'Super Cup' dhidi ya Chelsea.

Mane aliyeifungia Liverpool jumla ya mabao 45 tangu ajiunga na timu hiyo (2016), alisema kwa miaka saba sasa kwenye uchezaji wake soka, hajawahi kupata mapumziko ya zaidi ya siku 20.

"Kiukweli, nipo tayari kuanza. Nataka kuwajibika. Uchovu upo, lakini kilichopo mbele kitafanyika," alisema Mane.

Nyota huyo wa kimataifa wa Senegal alipewa wiki mbili za kupumzika baada ya kuifikisha timu yake ya taifa kwenye hatua ya fainali ya Mataifa ya Afrika 2019 Misri.

Winga huyo wa Liverpool amekosa michezo yote ya maandalizi ya msimu huu, ukijumuisha na mechi ya Ngoa ya Jamii ambayo walipoteza mbele ya Manchester City kwa mikwaju ya penalti.

Mane alianzia benchi kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England ambao Liverpool waliitandika Norwich City mabao 4-1, Ijumaa ya wiki iliyopita.