Manula, Kakolanya watoswa, Miraj ndani Taifa Stars ikiivaa Sudan

Monday September 16 2019

 

Dar es Salaam. Kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije amewaacha makipa wa Simba, Aishi Manula na Beno Kakolanya huku akimwita mshambuliaji wa Simba, Miraj Athumani katika kikosi chake kitakachoingia kambini kuivaa Sudan kusaka kufuzu kucheza CHAN2020, Cameroon.

Manula tangu alipoumia baada ya Afcon ameshindwa kupenya katika kikosi cha Ndayiragije, huku kipa wa Simba, Beno Kakolanya akiondolewa nafasi yake ikichukuliwa na kipa wa Yanga, Mechata Mnata.

Wengine waliondolewa katika kikosi hicho ni mshambuliaji Salim Aye wa KMC na pamoja na beki wa Yanga, Paul Godfrey wote ni majeruhi.

Mshambuliaji wa Simba, Miraj Athuman baada ya kufunga mabao mawili katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu ameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho  na ameungana na kipa wa Kagera Sugar, Mussa Kipao, Bakari Nondo wa Coastal Union, Mudathir Yahya kutoka Azam FC pamoja na Feisal Salum wa Yanga.

Wachezaji wengine waliotajwa makipa ni Juma Kaseja (KMC), Metacha Mnata (Yanga) na Kipao, mabeki wa pembeni Haruna Shamte (Simba), Boniface Maganga (KMC), Gadiel Michael na Mohamed Hussein 'Tshabalala' (Simba).

Mabeki wa kati Kelvin Yondan (Yanga), Erasto Nyoni (Simba), Idd Mobi (Polisi Tanzania) na Nondo, viungo ni Jonas Mkude na Mdhamiru Yassin (Simba), Baraka Majogoro (Polisi Tanzania), Mohammed Issa, Abdulraziz Makame na Feisal Salum (Yanga).

Advertisement

Wengine ni Idd Suleiman, Salum Aboubakary na Frank Domayo,  (Azam FC), washambuliaji ni Shaaban Idd (Azam FC), Ayoub Lyanga (Coastal Union), Hassan Dilunga na Miraji Athuman (Simba).

Fainali za CHAN zinatarajiwa kupigwa nchini Cameroon mwakani.

Mchezo wa kwanza utachezwa Septemba 22, na marudio Oktoba 18, Khartoum, Sudan mshindi wa jumla atafuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika nchini Cameroon mwakani.

Tanzania imefuzu kwa hatua hii baada ya kuing'oa Kenya katika mechi ya awali kwa mikwaju ya penalti baada ya kumaliza suluhu mechi zote mbili.

Advertisement