KIJIWENI LIVE : Eh! Masanja apata 'wakili' wa kumtetea msala wake Dodoma

VILE dunia imekamatwa na janga la ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi vya SARS Corona 2, basi supastaa Masanja Mkandamizaji akafanya kipindi kuwahoji wakazi wa Dodoma kuhusu uelewa wao.

Namna alivyowahoji kikomedi, DC Patrobas Katambi, akaagiza ajisalimishe polisi kwa kufanya utani kwenye mambo ‘serious’. Kijiweni ni mvutano, Luqman Maloto na Dk Levy wamegawanyika kama kawaida yao.

LUQMAN: Salamu ni tendo la kiungwana. Japo wewe si muungwana, acha nikusabahi. Umeshanawa mikono kwa sabuni, sasa ukiwa hapa kijiweni hakikisha ule mchezo wako wa kuchokonoa pua kwa kidole unaacha. Just grow up, bro!

DK LEVY: Dah mizuka yote ya kupiga stori na wewe imekatika. Umeongea kitu ambacho kila mtu huwa anafanya ila akifanya mwenzako ndo unakereka zaidi. Haya poa nimeshanawa mikono.

LUQMAN: Mwananchi wa Dodoma akiulizwa kuhusu Covid-19, akitoa jibu kuonyesha hajui. Tatizo ni la muuliza swali, mwananchi au aliyetakiwa kumfanya mwananchi ajue?

DK LEVY: Tatizo ni la mtu anayetumia lugha ya kigeni ambayo haijazoeleka. Kuuliza swali kwa watu ambao bila kutumia darubini utaelewa kuwa hawana uelewa huo. Ninaamini mpaka juzi kuna maofisa wengi wa Wizara ya Afya ambao hawakuelewa kirefu cha Covid-19.

LUQMAN: Sawa, tatizo ni la muuliza swali, muulizwaji au anayepaswa kuwafanya watu waelewe? Jibu kwa kifupi.

DK LEVY: Waelewe nini kupitia jina la kitaalamu? Muulizaji alifanya upuuzi tu kutaka watu wacheke. Angeuliza corona ndo angejua kama wanaelewa au hawaelewi. Wabunge wenyewe asilimia kubwa hawaelewi Covid-19 ni nini. Ujinga ni kutojua jambo, ila ujinga zaidi ni kudhani Wabongo hawana elimu au uelewa wa kutosha juu ya corona. Covid-19 naamini hata muulizaji hajui kirefu chake mpaka leo. Kamuulize mwanao corona ni nini kisha uje hapa kumtetea yule muhuni.

LUQMAN: Ukija nyumbani kwangu, ukamuuliza mtoto wangu “baba wa baba yako ni nani?” kishindwa kujibu, natakiwa nikugombeze kwamba kwa nini hukumuuliza “babu yako ni nani?” Nikulaumu kuwa swali lako lilimchanganya mtoto wangu?

DK LEVY: Na wewe ukija nyumbani kwangu ukamuuliza mwanangu kuwa TASAF ni nini badala ya kumfafanulia neno TASAF na umuhimu wake, nitakutandika mangumi matatu ya shingo. Wakati huu tunatakiwa kutumia kila fursa kusaidia watu kuwaelimisha juu ya corona. Sio kuleta komedi wakati kipindi chenyewe cha komedi kiliwashinda. Gademiti.

LUQMAN: Kwa nini usimweleweshe mwanao kuhusu Tasaf ili ajue? Sasa ukinipiga ngumi ndio utakuwa umemfanya mtoto wako ajue maana ya Tasaf? Unataka jamii ieleweshwe kuhusu corona, halafu unachukizwa na challenge za Masanja Mkandamizaji kuuliza watu kuhusu Covid-19. Wasipochafuka watajifunzaje? Ugonjwa unaitwa Covid-19. Unataka watu waendelee kukariri corona. Endelea kurusha ngumi, si unajiona Billy Blanks? Utopolo wewe.

DK LEVY: Mimi ningekuwa DC wa Dom bwana Katambi. Kwanza yule komediani angekuwa Segerea ya Dodoma. Ili utani wake akawapelekee wafungwa ambao wanahitaji faraja. Pili kile kijamaa kinachomtetea ningekipeleka huko huko wakakae pamoja. Huwezi kuleta mautani yako katika wakati kama huu. Kovidi naintiini mai futi.

LUQMAN: Mai futi mwenyewe. Uwe unaelewa. Alichokifanya Masanja ni safi sana. Watu wanasema corona, corona, corona. Sikiliza janga la dunia kwa sasa sio corona, ni covid-19. Na covid-19 ni maradhi yanayosabishwa na toleo namba mbili la virusi vya corona vinavyosababisha homa au mafua ya SARS, ndio maana virusi vinaitwa SARS Coronavirus 2 (SARS CoV2). Corona ni virusi vinavyotoka kwa wanyama na kusababisha magonjwa kwa binadamu (zoonotic diseases). Virusi vya corona vipo vya aina nyingi. Kuna virusi vya corona vinavyosababisha mafua ya SARS, vipo vyenye kuleta Homa ya Mashariki ya Kati (MERS), kuna hivi vya covid-19, pia Novel Corona. Mkuu wa Wilaya anatakiwa ahakikishe ujumbe unafika kwa watu wake. Umma uelewe. Sio kupambana na Masanja, utadhani yeye ndiye covid-19.

DK LEVY: Unatetea matango pori. Ushasema Homa ya Mashariki ya Kati. Sasa Dodoma ni Beijing? Unasema covid-19 ni tofauti na corona sasa wewe na yule mwehu mwenzako kawaambieni kwenye koo zenu kuwa corona ni tofauti na covid-19. Tanzania hasa Watanzania ndo watu pekee ambao wanaona ufahari na kumcheka mtu asiyejua kitu badala ya kumuelimisha. Unatumia lugha ya kitaalamu wakati wewe mwenyewe sio mtaalamu? Muulize huyo komediani wako, shuleni alikuwa anapata ngapi kwenye biology? Kama ilikuwa anapata biloo 50% aendelee kuchekesha walevi badala ya kuleta utani na vitu vya kitaalamu.

LUQMAN: Yaani covid-19 ni lugha ya kitaalamu? Hilo ndilo jina la ugonjwa. Ni kama malaria watu waseme ugonjwa ni parasite. Wakati parasite ni jamii ya wadudu. Kisha parasite anayeitwa plasmodium ndiye anayesababisha malaria. Au kipindupindu (cholera), ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria anayeitwa Vibrio Cholerae. Corona ni jamii ya virusi, sasa kirusi aina ya SARS Corona 2, ndio kinasababisha ugonjwa unaitwa covid-19. Tusiendelee kuchoshana, covid-19 ni jina la ugonjwa, watu wanapaswa kuelewa kuwa outbreak ya kidunia kwa sasa ni ugonjwa unaoitwa covid-19. Sio corona. Maana corona ni jamii kubwa ya virusi.

DK LEVY: Sasa unaona yule ndezi alikuwa anaelimisha au analeta utani na janga hili? Kwanza wewe mwenyewe kirefu cha UKIMWI nilikufafanuliwa 2011 pale viwanja vya Ustawi wa Jamii enzi za Vinega wa Anti Virus. Kama Ukimwi hukujua kirefu chake na umri ule vipi kuhusu AIDS utaelewa kweli? Angalia watu wa kuwafanyia utani kama ule. Ingekuwa wabunge ndo anawahoji na hawajui kitu kweli tungeshangaa na kucheka. Sio wanyonge wa Magufuli ndo wa kuwaletea utani. Sikia we Ndiefi hata rais wa nchi aliagiza kuacha utani na corona na DC alifuata agizo la rais. Sasa endeleeni.

LUQMAN: Kama mimi Ndiefi wewe Olembe. Bado nasisitiza Masanja hakukosea. Ugonjwa ni pandemic. Janga linalosambaa kwa kasi duniani. Watu hawajui. Masanja alifanya utani kwa sababu yeye ni mchekeshaji ili kufikisha ujumbe pakubwa. Watu wacheke, wengine wachotwe kwa kuulizwa na kushindwa kujibu, mwisho wajue kuwa ugonjwa ni covid-19 na sio corona. Tuache vitu vidogo, tupambane na covid-19, tuache kupoteza muda. DC Katambi badala ya kushughulika na Masanja, angeelewa kuwa elimu mahsusi haijafika kwa watu wake ndio maana hawajui ugonjwa unaitwa covid-19. Ukimuona Katambi mwambie namsalimia sana DC wetu wa Wilaya Kuu ya nchi. Si unajua Dodoma ndio Serikali inaishi. Ni kama Marekani Washington DC.

DK LEVY: Kuendelea kusema yule muhuni alikuwa sahihi ni kumkosea hadi mkuu wa nchi. Hiki kitu hakina utani. Tumeambiwa tusilete utani na corona. Angetumia neno corona unadhani kuna mtu asingemuelewa? Anatumia neno la kitaalamu kwa watu wale ili iweje? Halafu katania bila kutoa elimu yoyote mwishoni. Yaani kaweka utani na kuuacha kama ulivyo.