Mashabiki wa Arsenal wamcharukia mmiliki wa Klabu

Muktasari:

Tajiri huyo, Stan Kroenke aliyeanza kununua hisa za Arsenal mwaka 2007, amewahi kunukuliwa akisema hakununua klabu hiyo kwa lengo la kutwaa mataji.

Mashabiki wa Arsenal sasa wamechoshwa na vitendo vya mmiliki mwenye hisa nyingi za klabu hiyo, Stan Kroenke vinavyoifanya iporomoke na wamemuandikia waraka wakitaka aanze kuchukua hatua kuihuisha ili iwe na nguvu mpya.

Makundi makubwa ya mashabiki wa Arsena yameungana na kutoa taarifa hiyo kwa tajiri huyo Mmarekani, kwa mujibu wa yahoo.com.

Arsenal inajiandaa kushiriki michuano ya Europa kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kushindwa kumaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England katika nafasi nne za juu.

Na hadi sasa klabu hiyo kutoka kaskazinini mwa jiji la London imenunua mchezaji mmoja tu ambaye ni kinda Mbrazili, Gabriel Martinelli akiwa ni mchezaji pekee mpya katika kikosi cha Unai Emery.

Kwa sasa mashabiki wamechangikiwa kwa jinsi klabu hiyo inavyoendeshwa, huku wengi wakiamini kuwa Kroenke hana mpango wa kujaribu kupambana na klabu kama Manchester City na Liverpool ambazo sasa zimeiacha Arsenal mbali.

Bilionea huyo wa Marekani aliwasili Arsenal kwa mara ya kwanza mwaka 2007, ikiwa ni muda mfupi baada ya klabu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mwaka 2006 ilipofungwa na Barcelona mabao 2-1 jijini Paris.

Tangu wakati huo, Arsenal imefanikiwa mara tatu kutwaa ubingwa wa Kombe la FA na haijafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya tangu mwaka 2017.

Kushuka kwa kiwango uwanjani kumesababisha timu kucheza kwenye Uwanja wa Emirates huku maelfu ya viti yakiwa tupu kila wiki - na hali hiyo imesababisha mashabiki kuchukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza.

Kwa mara ya kwanza, makundi makubwa ya mashabiki, pamoja na watu wengine maarufu, tovuti na mabloga wameungana kutaka hatua zichukuliwe.

Wakitumia kaulimbiu ya #wecaredoyou (tunajali, wewe je), wametoa taarifa ya pamoja wakitaka Kroenke na klabu waanze kuangalia kuporomoka kwa timu katika miaka ya karibuni.

“Tukiwa mashabiki wa Arsenal tumeshuhudia tukiwa tumechanganyikiwa kuporomoka kwa kiwango cha soka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Wakati Stan Kroenke alipoanza kununua hisa za Arsenal, klabu ilishiriki kwa mara ya kwanza fainali ya Ligi ya Mabingwa. Miaka 12 baadaye, Arsenal inaelekea kushiriki Ligi ya Europa kwa mwaka wa tatu mfululizo," inasema taarifa hiyo.

“Nje ya uwanja, mashabiki wanajisikia kutokuwa na nguvu, wasiosikilizwa na wasio na thamani. Hii ilidhihirika wakati Stan Kroenke alipolazimisha kununua hisa zilizosalia za mashabiki bila ya hata kuonyesha heshima kwa nafasi yao katika klabu.

“Inaonekana kana kwamba Arsenal iko njiapanda. Mambo yanatakiwa yabadilike. Tunachokitaka sisi wote ambao tumesaini taarifa hii ni kuona hatua za maana zikichukuliwa na Stan Kroenke kuifufu klabu hii ya soka.

“Hii inahitaji kazi ya kuimarisha bodi ya klabu na wakurugenzi wa soka na kwa mara nyingine kuifanya Arsenal kuwa katika nafasi ambayo mashabiki watajisikia kuwa yao. Mabadiliko yanahitaji kuanzia na uongozi mpya.

“Katika nyaraka ya kuchukua klabu Stan Kroenke alisema: 'Lengo la KSE kwa klabu ni kuona inapambana mfululizo kutwaa ubingwa na Ligi ya Mabingwa'. Tunaona ushahidi mdogo wa jinsi ya kufikia hilo. Badala yake, klabu yetu inakuwa kama gari la uwekezaji, lililobinafsishwa na taarifa ya mmiliki kuwa hakuinunua Arsenal ili itwae ubingwa.

“Ni kitu kibaya taasisi kama Arsenal FC ina umiliki wa aina hiyo. Sisi wote tunataka tunataka kuona malengo na mwelekeo. KSE haina budi kuanza kwa kuwa na uwazi zaidi na uwajibiakji na kuelezea inakusudia vipi kufikia malengo ya kushinda mataji makubwa ya mchezo wa soka."