Kisa corona: Mashindano ya Olimpiki Tokyo 2020 yaahirishwa hadi 2021

Muktasari:

Olimpiki haijawahi kuahirishwa tangu kuanzishwa kwake miaka 124 iliyopita, japokuwa haikufanyika mwaka 1916, 1940 na 1944 kwa sababu ya vita mbili za duniani.

Tokyo, Japan. Michezo ya Olimpiki Tokyo 2020 imeahirishwa hadi mwakani kwa sababu ya janga la ugonjwa wa corona uliotikisa dunia kwa sasa.

Michezo hiyo ilitakiwa kuanza kufanyika Julai 24, 2020, lakini sasa imesogezwa mbele hadi mwakani 2021” imethibisha Shirikisho la kimataifa la Olimpiki (IOC).

"Tumekubaliana kuahirisha kwa mwaka moja na rais wa IOC, Thomas Bach amekubali kwa asilimia 100%," alisema Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe.

Pia, Michezo ya Tokyo Paralympic imesogezwa mbele hadi 2021.

Michezo hiyo itaendelea kuitwa Tokyo 2020 pamoja na kuwa itafanyika 2021, ilisema IOC.

Katika taarifa ya pamoja kati ya waandaji wa Tokyo 2020 na IOC ilisema: "Kumetokea jambo ambalo hakuna aliyetegemea kuona namna ugonjwa huu unavyosambaa kwa kasi duniani kote.

"Jumatatu mkurungezi wa Shirika la Afya Dunia (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema COVID-19 ni janga.

"Kuna wagonjwa zaidi 375,000 duniani kote karibu kila nchini na idadi imekuwa ikiongezeka kila saa.

"Kutokana na hali ya sasa na taarifa ya WHO ya leo (Jumanne), rais wa IOC na waziri mkuu Japan wamekubaliana  kubadilisha tarehe ya kufanyika kwa Tokyo Olimpiki kutoka 2020 hadi 2021, kwa ajili ya kulinda afya na usalama wa wanamichezo na wote jamii ya kimataifa."

Olimpiki haijawahi kuahirishwa tangu kuanzishwa kwake miaka 124 iliyopita, japokuwa haikufanyika mwaka 1916, 1940 na 1944 kwa sababu ya vita mbili za duniani.

Wakati wa vita baridi baadhi ya nchi ziligomea kushiriki mashindano ya Moscow na Los Angeles kati ya mwaka 1980 na 1984.