Masoud ashindwa kujizuia

Muktasari:

  • Masoud aliyekuwa kwenye kikosi cha Simba kilichoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akisaidia na Pierre Lechantre na kutolewa na Al Masry ya Misri katika raundi ya kwanza, alimuuma sikio Aussems ili mambo yaende sawa Msimbazi.

MABOSI wa Simba walimpiga chini aliyekuwa kocha msaidizi wa timu yao, Masoud Djuma kwa kumvunjia mkataba Oktoba mwaka jana kwa maagizo ya Kocha Patrick Aussems tena bila kutarajiwa na baadhi ya mashabiki wakaamini huenda jamaa huyo atakuwa na kinyongo nao.

Hata hivyo, licha ya kuachana na Simba katika mazingira yasiyo ya kirafiki, lakini kumbe anaendelea kuifuatilia timu hiyo kwa kila inachokifanya japo kwa sasa maisha yamemchanganyia kule Rwanda anakokinoa kikosi cha AS Kigali.

Sasa unaambiwa kipigo cha mabao 5-0 ilichopewa Simba na wapinzani wao wa Kundi D, AS Vita katika Ligi ya Mabingwa Afrika kimemfanya Mrundi huyo kuvunja ukimya huku akimpa akili bosi wake wa zamani, Patrick Aussems namna ya kwenda kuifanyizia Al Ahly kwao, Misri.

Masoud aliyekuwa kwenye kikosi cha Simba kilichoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akisaidia na Pierre Lechantre na kutolewa na Al Masry ya Misri katika raundi ya kwanza, alimuuma sikio Aussems ili mambo yaende sawa Msimbazi.

Akiwa anakumbuka waliondolewa michuanoni kwa sheria ya faida ya bao la ugenini baada ya kulazimishwa sare nyumbani ya mabao 2-2 na kutoka suluhu mjini Cairo, Masoud alisema kipigo cha Kinshasa lazima kisahaulike na sasa Aussems na jeshi lake wajipange kwa Waarabu.

Alisema kitu cha kwanza Aussems na Simba yake wanachotakiwa kufanya ni kusahau kufungwa mabao mengi katika mechi ya AS Vita ili kurekebisha makosa yote waliyofanya kwenye mchezo huo kwani wanaenda kukutana na kigogo kingine.

Mrundi huyo alisema kama Simba itaendelea kukumbuka matokeo hayo ya Kinshasa, basi wajue wazi wanaweza kujikuta wakipoteza mechi zaidi hasa hiyo inayofuata dhidi ya Al Ahly.

“Kwanza wanatakiwa kuwa na mahesabu makali ya kupata pointi hata moja mchezo wowote wa ugenini, kwani timu yao ina uwezo wa kupata pointi tisa nyumbani, hivyo watamaliza kundi wakiwa na pointi 10 ambazo zitawavusha moja kwa moja hatau ya robo fainali,” alisema.

“Lakini wakisema washinde mechi zote za nyumbani bila wao kupata hata pointi moja ugenini wanaweza kumaliza mechi katika kundi wakiwa pointi sawa na AS Vita ambao watakuwa na matokeo mazuri katika sheria ile ya kukutana wenyewe kwa wenyewe na wao watasonga.”

“Kingine wanatakiwa kujitahidi ili wapate ushindi mechi mbili zilizobaki watakazocheza nyumbani, ila kama watapata matokeo yoyote tofauti na pointi tatu hawana nafasi ya kufuzu tena kwani kila timu katika mashindano haya lazima watataka ushindi wakiwa kwao,” alisema.

Masoud alisema Simba inatakiwa kuwa na heshima kubwa wanapocheza mechi za ugenini kwani wakienda na mbinu yao ya kushambulia mwanzo mwisho hawataweza kupata hata pointi moja kwani timu walionao kundi lao ni kubwa na zina uwezo mkubwa.

Kocha huyo aliyekuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba, alitemwa Msimbazi baada ya Kocha Aussems kumuacha nje ya kikosi chake kilichosafiri mechi za mikoani ikielezwa hawakuwa wakiiva, huku mkataba wake ukisalia muda wa mwaka mmoja kwani ulikuwa wa miaka miwili ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi.