Mastaa Man United wakorogana kisa kipigo cha Everton

London, England. Malumbano makali yameibuka ndani ya vyumba vya kuvalia nguo muda mfupi baada ya Manchester United kuchapwa mabao 4-0 na Everton.

Habari za ndani zimedai mzozo mkubwa uliibuka baada ya kila mmoja kumnyooshea kidole mwenzake akidai ndio chanzo cha kubugizwa idadi kubwa ya mabao.

Pia Kocha Ole Gunnar Solskjaer alitumia muda mfupi na wachezaji akionyesha kuchukizwa na kiwango kibovu cha Man United katika mchezo huo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Goodison Park, Jumapili iliyopita.

Ingawa kocha huyo aliomba radhi kwa mashabiki, lakini alichukizwa na kitendo cha Man United kucheza chini ya kiwango na ameahidia kufumua kikosi hicho katika usajili wa majira ya kiangazi.

Ndani ya vyumba vya kuvalia nguo hali ilikuwa tete kwani kila mmoja alimtaja mtu aliyedhani alikuwa chanzo cha kupata kipigo hicho cha aibu tangu kocha huyo alipotwaa mikoba ya Jose Mourinho.

Paul Pogba alisema hali ilikuwa mbaya kwa kuwa kila mchezaji, ofisa na kocha walitoa maneno makali.

“Hatukujitendea haki wenyewe ndani ya uwanja, klabu na mashabiki. Kocha alizungumza na maofisa waliongea ukweli,” alisema nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa.

Solskjear na msaidizi wake Mike Phelan walifanya kikao cha dharura ambacho kililenga kupangua kikosi na kuongeza nyota wapya katika usajili wa majira ya kiangazi.