Mbappe aongoza kura za kukipiga Real Madrid

Muktasari:

 

 

  • Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, yuko katika presha kubwa ya kutumia pesa nyingi katika dirisha kubwa la uhamisho baada ya Real Madrid kuyumba msimu huu wa michuano mbalimbali huku akishindwa kuziba pengo la staa wake, Cristiano Ronaldo, ambaye aliuzwa kwenda Juventus katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka jana kwa dau la pauni 88 milioni.

MADRID,HISPANIA .HATUTAKI ujinga. Ndivyo inavyoonekana walichoamua mashabiki wa Real Madrid. Baada ya timu yao kudorora msimu huu, wameamua kwenda mitandaoni kupiga kura za kuitaka klabu yao kuwanunua baadhi ya mastaa nyota katika dirisha kubwa lijalo la uhamisho.

Majina ya Kylian Mbappe wa PSG, Paul Pogba wa Manchester United, Matthijs de Ligt wa Ajax na Eden Hazard wa Chelsea yameonekana kupigiwa chapuo katika kura za mashabiki wa Real Madrid zilizoendeshwa na gazeti maarufu la michezo nchini Hispania, Marca.

Zaidi ya mashabiki 200,000 walipiga kura hizo na jina la Mbappe lilionekana kuteka hisia za mashabiki wa timu hiyo maarufu zaidi duniani ambako asilimia 79 ya kura zilikwenda kwa Mbappe mbele ya nyota wengine kama staa mwenzake wa PSG, Neymar pamoja na staa wa Tottenham, Harry Kane.

Mashabiki hao waliambiwa wachague wachezaji wanaowataka katika nafasi tofauti ambako katika nafasi ya ulinzi waliwekewa majina kama ya mlinzi wa Ajax, Matthjis De Ligt, mlinzi wa Inter Milan, Milan Skriniar, na mlinzi wa Napoli, Kalidou Koulibaly ambaye jina lake limekuwa likihusishwa zaidi na Manchester United.

Katika kura za eneo la ulinzi, De Ligt ambaye ni nahodha wa Ajax akiwa na umri wa miaka 19 tu aliwakimbiza wenzake na kupata asilimia 67 ya kura zote. Hata hivyo, kinda huyo amekuwa akihusishwa zaidi kwenda kwa wapinzani wa Real, Barcelona alikotangulia nyota mwenzake Frenkie De Jong.

Kwa upande wa walinzi wa pembeni, Chelsea inabidi ikae mkao wa kuvamiwa baada ya jina la mlinzi wao wa kushoto, Marcos Alonso, kupata kura nyingi mbele ya mlinzi wa kushoto wa Bayern Munich, David Alaba, ambaye awali ilidhaniwa angeweza kuibuka mshindi.

Katika eneo la kiungo, staa wa Manchester United, Paul Pogba, ambaye katika siku za karibuni alikaririwa na vyombo vya habari akidai kwamba Real Madrid ni timu ya ndoto zake, alionekana kuwaburuza wenzake katika eneo hilo.

Jina lake lilipata kura nyingi mbele ya mastaa wenzake kama vile kiungo wa Lazio na timu ya taifa ya Serbia, Sergej Milinkovic-Savic, nyota wa Bayern Munich, Thiago Alcantara, na kiungo mahiri wa Juventus Turin, Miralem Pjanic.

Kwa upande wa mawinga, staa wa Chelsea, Eden Hazard, ambaye ameonekana kuhusishwa zaidi kwenda Real Madrid katika dirisha kubwa la majira ya joto, alipata kura zaidi ya asilimia 70 na kumpita staa wa Tottenham, Christian Eriksen, ambaye pia amekuwa akihusishwa kwenda klabuni hapo.

Katika majina yote haya, mashabiki wamesisimkwa zaidi na Mbappe ambaye miaka michache iliyopita alikuwa kinda zaidi katika klabu ya Monaco huku tayari baadhi ya washambuliaji waliowekwa katika orodha yake akina Kane, Neymar, Mauro Icardi na Pierre-Emerick Aubameyang wakiwa majina makubwa.

Mbappe pia amekuwa akihusishwa kwenda Real Madrid ambako kama dili lake likitimia basi atavunja rekodi ya uhamisho ya dunia ambayo ilikwenda na Neymar katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka 2017.