Mbappe avunja rekodi za mabao ya Messi, Benzema Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:

Mbappe amefikisha idadi ya mabao 15, akiwa na umri wa miaka 20 na siku 306 wakati Messi alifanya hivyo alipokuwa na umri wa miaka 21 na siku 288

Paris, Ufaransa. Mabao matatu ya Kylian Mbappe katika ushindi wa mabao 5-0 iliyopata Paris St Germain dhidi ya Club Brugge yamemfanya kinda huyo mwenye umri wa miaka 20 kuivunja rekodi Lionel Messi na Karim Benzema katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbappe ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufikisha idadi ya mabao 15 katika mashindano hayo akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Messi.

Mbappe amefikisha idadi hiyo ya mabao akiwa na umri wa miaka 20 na siku 306 wakati Messi alifanya hivyo alipokuwa na umri wa miaka 21 na siku 288 ambapo ilikuwa ni Aprili 8, 2009 katika mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ambapo Barcelona waliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Mbali ya rekodi hiyo Mbappe pia amevunja rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kufikisha umri wa miaka 21 ambapo awali ilikuwa inashikiliwa na Karim Benzema.

Mbappe amefunga mabao 17 kwenye mashindano hayo kabla ya kufikisha miaka 21 wakati Benzema alipachika jumla ya mabao 15.

Kwa upande mwingine, nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos ameweka rekodi ya kuwa beki aliyecheza idadi kubwa ya michezo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwemo katika kikosi cha timu hiyo kilichoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Galatasaray.

Ramos amecheza jumla ya mechi 121 hadi sasa za Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu alipoanza kuichezea Real Madrid mwaka 2015.